Kampuni mama ya Google, ALPHABET inaweza kuipita kampuni ya Apple na kuwa kampuni yenye thamani kubwa zaidi duniani. Mwaka 2015 ulikua ni mwaka wa matukio mengi kwa Google, hii ikiwa ni pamoja na mabadiliko mbalimbali kufanyika.
Mwaka huo tuliona kampuni hiyo ikibadili logo na kugawanywa na kuwa kampuni moja kati ya kadhaa zote zikiwa chini ya kampuni mama mpya iliyopewa jina la ALPHABET.
Watafiti wa mambo ya kiuchumi – hisa na mapato wanaona ya kwamba kwa mwaka huu kampuni ya ALPHABET ipo njiani kuwa na mabavu makubwa . Kumbuka pia mambo hayaendi vizuri kivile katika kampuni la Apple ambapo mapato yake mengi yanategemewa kutoka katika uuzaji wa simu, na tayari inaonekana simu hizo haziitajiki kwa kasi kwenye soko kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kulingana na kampuni ya Ushauri IDC, imesema kuwa soko la simu janja limeshuka kwa asilimia 10 mwaka uliopita. Watafiti wana mawazo kuwa kampuni inaweza ikawa na kibarua kigumu mwaka huu katika kuhakikisha kuwa mauzo ya iPhone yanalingana milioni 230 (mauzo ya mwaka jana) au zaidi.
Kumbuka mauzo hayo yanaweza yasifikiwe kwa kuwa soko la simu janja limekuwa kubwa sana. Kuna machaguo mengi , kwa mfano Android ikikuboa una uwezo mkubwa wa kuhamia katika Apple n.k. Na nje ya machaguo ni kwamba watu wengi wanamiliki simu janja bora kipindi hiki na hivyo hawajisikii ulazima wa kubadilisha simu kila baada ya miezi sita au mwaka na hivyo matoleo mapya ya simu za iPhone yanakuwa hayauzi sana kama zamani.
Pia ukubwa wa soko hili unaweza hata ukashusha bei za simu kazaa (kama ni bei kubwa, wachache watanunua). Kampuni ya Apple inapata asilimia 60 ya mapato yake katika uuzaji wa simu, watafiti wengi wanategemea maendeleo madogo kwa kampuni ya Apple kwa mwaka 2016.
Kwa upande mwingine kampuni ya ALPHABET bado ndio mfalme wa matangazo kupitia huduma ya Google Ads. Mshauri wa soko la mtandaoni amekadiria kuwa matangazo ya simu ya kimtandao yatajiongeza mara mbili na kuelekea dola bilioni 200 za kimarekani mnamo mwaka 2019. Kwa kiasi kikubwa watu wengi hasa katika nchi zinazoendelea wanamiliki simu kwa mara ya kwanza na hivyo soko la matangazo ya kimtandao linazidi kukua.
Mapato ya kampuni la ALPHABET yanatemewa kupanda kwa asilimia 15 mwaka huu. Kumbuka kuna bidhaa kama magari ya kujiendesha yenyewe, Roboti za siri, na huduma ya intaneti yenye kasi ya ajabu, bidhaa zote hizi zinaonesha kwa kina kuwa kampuni hii ina milango mingi ya kupata mapato zaidi ikilinganishwa na Apple wanaotegemea mauzo ya iPhone zaidi.
Kampuni ya ALPHABET linategemea sana katika matangazo ya kimtandao kuliko Apple katika iPhone. Matangazo ya kimtandao yanalipatia kampuni ya ALPHABET mapato ya asilimia 90.
Yote tisa kumi ni kwamba kampuni ambalo litapata mapato mengi ndilo litakalobaki kileleni kama kampuni lenye hadhi na thamani zaidi duniani. Kumbuka makampuni haya mawili ni makampuni makubwa duniani na ni makampuni ambayo watu wengi wanategemea yatakuwa na ushindani zaidi kwa mwaka huu.
No Comment! Be the first one.