Mtandao wa Facebook unazidi kukua na kutunisha misuli katika biashara ya matangazo ya kimtandao. Na ukuaji wake katika nchi zinazoendelea ukizidi kuchangia kwa kasi ukuaji wake.
Katika ripoti iliyotolewa na mwanzilishi na Mkurugenzi mkuu wa Facebook, Bwana Mark Zuckerberg, inaonesha mtandao huo unazidi kukua kwa kasi nzuri.
Ukuaji wa watumiaji
Kufikia tarehe 27 ambapo ripoti ya mtandao huo umetoka rasmi inaonesha mtandao huo una idadi ya watumiaji bilioni 1.59 kila mwezi.
Kwa wakati huo huo kwa wastani mtandao huo una watumiaji bilioni 1.04 kila siku, imekua ukilinganisha na wastani wa watumiaji bilioni 1.03 kwa siku kati ya mwezi wa saba hadi wa tisa mwaka 2015.
Mwaka 2015 watumiaji wa mtandao huo kwa mwezi walikua kwa asilimia 14 ukilinganisha na idadi ya watumiaji mwaka kabla yake.
Ukuaji wa kipato
Mtandao huo katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa 2015 (Q4) ulifanikiwa kuingiza $ bilioni 5.841 (Takribani Tsh 12,791,497,950,000/= | Kes 597,472,969,500/=. Huu ni ukuaji mkubwa ukilinganisha na mapato ya dola bilioni 5.841 za Marekani katika kipindi cha miezi mitatu (Q3) kabla (Julai – Septemba 2015).
Inaonekana Facebook wanatengeneza pesa kwa kasi kubwa kuliko kasi ya kupata watumiaji wapya.
Watumiaji kutoka mataifa yanayoendelea na watumiaji wa simu za mkononi!
Pia data zinaonesha ya kwamba maendeleo ya kupata watumiaji wapya nje ya bara la Amerika na Ulaya yakizidi kuchangia ukuaji wake wa mapato.
Kingine kilichoonekana katika ripoti hiyo ni kwamba watumiaji wa Facebook kupitia simu za mkononi wanazidi kuchangia mapato zaidi kwa kampuni hiyo ukilinganisha na watumiaji wa kompyuta. Asilimia 80% ya mapato ya Facebook kupitia huduma yake ya matangazo yanatokana na watumiaji wa huduma hiyo kupitia simu za mkononi (Mobile).
Watumiaji wa Facebook kupitia simu ya mkononi ni takribani milioni 827 kwa mwezi.
Data zingine
Mark Zuckerberg alitoa data zingine za utumiaji wa huduma za Facebook katika kipindi cha Q4 ya 2015 (Septemba – Disemba) kama ifuatavyo;
- Idadi ya masaa milioni 100 ya utazamaji wa video katika Facebook kwa siku
- Huduma ya Groups (Makundi) ya Facebook ina watumiaji bilioni 1
- Toleo lao la app ya Facebook isiyotumia data nyingi (Facebook Lite) imefikisha idadi ya watumiaji milioni 80
- Huduma yao ya upangaji wa matukio (Events) ilitumiwa na watumiaji milioni 500
- Matukio milioni 123 yaliwekwa katika huduma ya Events kwa mwaka 2015
- Biashara ndogo na ukubwa wa kati takribani milioni 50 zinatumia huduma yake ya Pages (Kurasa spesheli).
Kwa wastani Facebook imeingiza Dola $3.73 kwa kila mtumiaji mmoja katika kipindi cha Septemba – Disemba (2015). Hii ni takribani Tsh 8,160/= | Kes 381/=
Huduma ya Facebook inazidi kukua ingawa inaonekana tayari ukuaji umepungua katika nchi zilizoendelea.
No Comment! Be the first one.