Je umeshatamani kuwa na diski (External) kwa ajili ya kuhifadhi data zako kiusalama zaidi? Fahamu kuhusu diski za SecureDrive KP.
Diski hizi zinahitaji mtu kuingiza nywila yake ili kuweza kufanya kazi. Yaani kama hauna password basi diski nzima haisomi kwenye kompyuta yako.

Watengenezaji na wauzaji wa diski hizi, SecureDrive, wamezitengeneza katika ujazo mbalimbali.
Kupitia teknolojia ya HDD – Kuna toleo la:
- TB 1 ($275 / Tsh 640,000) na
- TB 2 ($329 / Tsh 762,000).
Kupitia teknolojia ya SSD kuna matoleo ya:
- GB 250 ($309 / Tsh 715,000),
- GB 500 ($385 / Tsh 890,000),
- TB 1 ($549 / Tsh 1,270,000),
- TB 2 ($959 / Tsh 2,220,000),
- TB 4 ($1,869 / Tsh 4,325,000) na
- TB 8 ($3,629 / Tsh 8,400,000).
*Kumbuka bei hizi ni kwa Marekani, na hivyo upatikanaji wake huku unaweza kufanya bei yake iwe juu zaidi kidogo. Fahamu kuhusu tofauti ya teknolojia ya HDD na ile SSD kwa kusoma hapa -> Teknokona / Tofauti ya HDD na SSD
Diski hiyo ikigundua mtu anajaribu kufanya udukuzi, kwa kujaribu kudanganya nywila n.k, unaweza kuweka mpangilio/setting ya kufanya diski hiyo ijifute data.
Pia unaweza kuweka mpangilio wa kuruhusu watu kusoma tuu data na si kuweka kitu (Read Only). Ndani yake imetumika teknolojia ya kuhakikisha ata mtu akijaribu kuifungua basi ndio itaharibika kabisa na hivyo mtu kushindwa kabisa kujaribu kuiunganisha kimaujanja ili kusoma data zake.