Apple ni kampuni kubwa kiteknolojia inayojihusisha na utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki pamoja na programu endeshi zake. Teknokona leo tunakuletea orodha ya vifaa vya kielektroniki vinavyo tengenezwa na Apple.
Kampuni ya Apple ni moja kati ya kampuni kubwa 5 za teknolojia ya mawasiliano nchini Marekani zingine zikiwa ni Alphabet, Meta, Amazon na Microsoft. Apple wamekuwa wakijivunia kutengeneza bidhaa nyepesi kutumia na zenye ulinzi wa kutosha dhidi ya wadukuzi na sifa hizi ndizo zilizolikuza soko la bidhaa za Apple kwa wateja wake. Vifaa vya kielektroniki vinavyotengenezwa na Apple ni pamoja na:
iPhone: Apple walianza kutengeneza simu janja mwaka 2007 na kuzipa jina la iPhone ambapo toleo lao la kwanza lilikuwa ni iPhone 3. Pia kampuni ya Apple ilihusika na utengenezaji wa programu endeshi za simu janja zake ambayo ni iOS, kutokana na ukuaji wa teknolojia uliokuwa ukiendelea katika miaka iliyofuata kampuni ya Apple iliendelea kuboresha simu janja zake kupitia matoleo mbalimbali. Toleo jipya la sasa ni iPhone 13 inayotumia programu endeshi ya iOS 15.

iPad: Ni kifaa cha kielektroniki chenye umbo la ubao (Tablet), matumizi ya kifaa hiki cha Apple hayana tofauti sana na simu janja ila tu kifaa hiki ni kikubwa zaidi kiumbo. Apple walianza kutengeneza iPad mwaka 2010 na baada ya hapo wakawa wanatoa matoleo mbalimbali ya kifaa hiki cha kielektroniki huku wakiyagawa matoleo hayo katika makundi tofauti kulingana na uwezo wa toleo hilo pamoja na vigezo vingine vingi. Makundi hayo ya matoleo ya iPad ni iPad mini,iPad Air na iPad Pro na zote zikiwa zinatumia programu endeshi ya iPadOS.
Mac mini: Hii ni moja kati ya komyuta za mezani zinazotengenezwa na Apple. Kompyuta hii ya mezani inakuja kama kiboksi kidogo chenye matundu ya kuchomekea nyaya kwaajili ya kuunganisha na skrini ya komyuta unayotaka kuonyeshea. Apple waliamua kutengeneza kompyuta hizi za mezani ili kuziba pengo la wateja wao wasioweza kununua komyuta zao za mezani zenye skrini kutokana na ukubwa wa bei. Kifaa hiki cha kielektroniki kilianza kutengenezwa na Apple mwaka 2005 na kuboreshwa kupitia matoleo mbalimbali pia Mac mini hutumia programu endeshi ya Mac OS X.

MacBook: Apple walianza kutengeneza kompyuta mpakato aina ya MacBook mwaka 2006. Kutokana na mahitaji ya wateja wao kuwa tofauti Apple waliamua kuunda makundi mawili tofauti ya matoleo ya MacBook ambayo ni MacBook Air na MacBook Pro. Tofauti iliyopo kati ya matoleo ya MacBook Air na MacBook Pro ni uwezo wa kompyuta hizo pamoja na ukubwa wa umbo. MacBook Pro ni kubwa kiumbo na pia kiuwezo lakini MacBook Air ni ndogo kiumbo na pia kiuwezo ukilinganisha na MacBook Pro. Kompyuta mpakato zote za MacBook zinatumia programu endeshi ya Mac OS X.
No Comment! Be the first one.