Kirusi cha Melissa kilikuwa ni kirusi cha kompyuta maarufu kilicholeta matatizo makubwa katika mawasiliano barua pepe mwaka 1999. Kirusi hicho kilianza kusambaa kupitia mifumo ya mawasiliano ya barua pepe (email) mwezi Machi mwaka 1999.
Kirusi cha Melissa kilikuwa na nguvu sana na kililazimisha Microsoft na kampuni nyingine kubwa kuzima mifumo yao ya barua pepe hadi kirusi huyo kudhibitiwa kwanza.
Alisambaaje?
Kirusi huyo alisambaa kupitia barua pepe. Barua pepe ilikuwa ikitumwa kwa mtu ikimuonesha kuna faili muhimu la kufungua lililokuja na barua pepe hiyo (attachment). Kitendo cha kufungua tuu basi kirusi cha Melissa kinaingia kwenye kompyuta husika, na kisha kinatuma barua pepe zingine kwa watu 50 walio kwenye mfumo wa anuani ya akaunti ya barua pepe husika. Programu za Microsoft Outlook 97 na 98 ndio ziliathirika zaidi.
Kirusi hicho kilileta shida kubwa katika mifumo ya barua pepe kwani mifumo mingi ilikuwa inaelemewa na hivyo kusababisha mawasiliano ya barua pepe yawe kwa shida katika kipindi hicho.
Mtengenezaji
Shirika la usalama la FBI la Marekani lilifanikiwa kumkata Bwana David L Smith, kijana wa miaka 30 wa jiji la New Jersey. Kumkata kwake kulihusisha ufuatiliaji wa barua pepe ya kwanza iliyotuma kirusi hicho, na pia ilihusisha huduma ya intaneti na barua pepe ya AOL walioweza kuonesha jinsi mteja wao mmoja alidukuliwa, na uchunguzi wa udukuzi huo ndio uliwafikisha FBI kwa Bwana Smith.
Inasemekana ingawa kitendo chake kilisababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 80, pesa nyingi sana kwa wakati huo, Bwana Smith aliweza epuka kifungo cha muda mrefu kutokana na kutoa ushirikiano kwa FBI katika ukamataji wa wadukuzi wengine. Bwana Smith alitumikia kifungo cha miezi 20 tuu jela.
Kirusi cha Melissa bado kinashika sifa ya kuwa moja ya kirusi cha kwanza kilichofanikiwa zaidi katika udukuzi wa mfumo wa barua pepe duniani. Kilileta changamoto kubwa katika mifumo ya usalama wa barua pepe, siku hizi ni vigumu zaidi udukuzi wa namna hii kusambaa kutokana na teknolojia za kiusalama zilizoboreshwa zaidi katika mifumo ya barua pepe.
No Comment! Be the first one.