Kuwa na huduma ya Intaneti ya bure kwa mtanzania pengine ni kitu anachotamani kila mmoja wetu kiwepo. Lakini hilo laonekana kama ndoto za mchana na lisilowezekana kwa nchi za ukanda wetu.
Kwa nchi za Ulaya si jambo la ndotoni bali ni halisi na linalowezekana.
Kamati ya Umoja wa Ulaya imetangaza kutoa huduma bure za WiFi katika maelfu ya miji ya nchi za Umoja wa Ulaya. Wakazi na watalii watanufaika na mpango huo wa mtandao wa intaneti uitwao “WiFi 4 EU”.
Tarehe 29 mwezi Mei kamati ya EU, baraza la EU na bunge la Ulaya wameafikiana kuhusu mpango huo na chanzo cha fedha kwa ajili ya mpango huo.
Mpango huo utakusanya kiasi cha Euro milioni 120 katika miaka miwili ijayo, na kuanza kutoa huduma bure za Wifi katika bustani, viwanja, maktaba, vituo vya afya, majumba ya makumbusho na maeneo mengine ya umma kwenye miji 6000 hadi 8000.
Mpango huo ni hatua mpya ya mkakati wa utandawazi wa soko la dijitali. Ili kusukuma mbele mkakati huo, mwezi Februari mwaka huu Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa kuanzia tarehe 15 Juni, watu wanapopiga simu, kutuma ujumbe au kutumia mtandao wa Interent kupitia simu za mkononi wakati wanaposafiri katika nchi nyingine za umoja huo, hawatatozwa gharama ya ziada – yaani ‘roaming fees’.
Aidha, mwezi uliopita bunge la Ulaya liliidhinisha kanuni mpya ikiamua kwamba wateja wakisajili huduma za kusoma habari mbalimbali kupitia mtandao wa intaneti katika nchi moja, wakienda nchi nyingi za umoja huo, pia hawahitaji kulipa tena.