Moja ya huduma maarufu ya barua pepe nchini Marekani, VFEmail.net imedukuliwa na wadukuzi na kufutiwa data zote za watumiaji wake.
Huduma ya barua pepe ya VFEmail imekuwa ikijijengea sifa kama huduma ya barua pepe ya kulipia ambayo ni salama kwa watumiaji wake – ikiwahakikishia ulinzi dhidi ya udukuzi wa data.

Tarehe 11 mwezi huu huduma hiyo ilidukuliwa na wadukuzi waliweza kupata uwezo wa kuingia kwenye kompyuta mama za huduma hiyo (servers) za nchini Marekani. Hadi sasa kampuni ya VFEmail imeshindwa kabisa kurudisha data za watumiaji wake na wanaamini mdukuzi/wadukuzi hao walifuta data za kwenye servers.
Ubaya ni kwamba hawakuishia kwenye servers moja bali walidukua hadi kompyuta mama za dharula (backup) na kufanya yale yale – kufuta data zote.

Ni kawaida wadukuzi wakifanikiwa kudukua kompyuta mama/server za tovuti kufanya mawili;
- Kuitumia nafasi hiyo ya kompyuta kwa ajili ya vitu vyao wenyewe
- Kuwazuia watu wapya kutembelea tovuti hiyo (DDoS)
- Kuwazuia wenye tovuti kuweza kuingia eneo la kufanya mabadaliko (Admin) na kudai pesa kwanza ili kuweza kurudisha uwezo huo.
Ila mdukuzi huyu hakutaka hayo, yeye alifuta data zote za huduma hiyo kwa watumiaji wa nchini Marekani. Inasemakana kwa asa VFEmail wamefanikiwa kurudisha akaunti za watu ila watu hao wakiingia kwenye barua pepe zao watakuta ni kama mpya. Barua pepe zao zote za zamani hazipo – hii data yote imepotea.
VFEmail wanasema bado wanajaribu njia mbalimbali kuona kama wataweza kuokoa data za aina yeyote – ila kwa ufupi ata wao wenyewe wanaonekana wamekata tamaa kiasi flani.
VFEMail – https://www.vfemail.net/