fbpx
TeknoKona Teknolojia Tanzania
Intaneti Tanzania Teknolojia

Uchambuzi: Nimetumia Halotel Kwa Siku Kadhaa, Fahamu Nilichokutana Nacho

Uchambuzi: Nimetumia Halotel Kwa Siku Kadhaa, Fahamu Nilichokutana Nacho

Spread the love

Katika miaka ya hivi karibuni imeingia mitandao mingi ya simu nchini na kudumu wakati mingine ikapotea baada ya muda mchache na mingine bado ipo ila inaishi kwa ‘dripu’ – yaani hali ngumu. Najivunia kwa kufanikiwa kutumia huduma za mitandao karibia yote nchini na hivyo kuweza kutoa tathmini nzuri ya mtandao mmoja pale ninapolinganisha na mingine yote.

‘Nilijiunga mtandao wa Sasatel mara moja tuu ulivyoanza kutoa huduma – mtandao huo kwa sasa ni historia na sishangai, niliachana nao kabla haujafa. Nina uhakika mtandao wa Halotel utafanikiwa haraka ata kuupita mwingine mpya -Smart  upo nchini muda mrefu tu kwa sasa lakina haujapiga kelele za kutosha’

Kingine kikubwa kitakachowapa mafanikio ya haraka ni upana wa upatikanaji wa minara yao karibia nchi nzima

Kingine kikubwa kitakachowapa mafanikio ya haraka ni upana wa upatikanaji wa minara yao karibia nchi nzima

Jumatano nilifanikiwa kununua laini pamoja na vocha ya buku kumi ya mtandao mpya wa simu wa Halotel, kutokana na uwekezaji mkubwa waliokuwa wamekwishaufanya na kufahamika sikuwa na wasiwasi sana na kiwango cha huduma yao ila bado nikawa nimejiaminisha nitaujaribu kwa angalau siku kadhaa alafu niamue kama niendelee kutumia au niachane nao. Na leo ikiwa takribani siku 3-4 tokea nianze kuutumia mtandao huo rasmi basi ningependa kutoa tathmini yangu kwa wengine ambao tayari wamekuwa wakiufikiria.

Nitaelezea vyote kwa mfumo wa muda, na uchambuzi huu utakuwa mrefu ila ni muhimu kuwa huru na kutojinyima kusema yote kwa sababu ya urefu. 🙂

Siku ya kwanza

Niliingia na kununua laini yangu mpya ya Halotel katika duka lao lililopo barabara ya Bagamoyo karibu na kituo cha mafuta cha Victoria, jengo la AAR. Wahudumu walikuwa wachangamfu na nilipoulizia kama wanatoa namba spesheli, yaani chaguo langu walisema ndio na ingenigharimu elfu 2. Nilipata laini hiyo hapo baada ya hatua za usajili wa laini hiyo kufanyika fasta fasta.

Laini ya Halotel - tayari laini zishaanza kupatikana sehemu mbalimbali

Laini ya Halotel – tayari laini zishaanza kupatikana sehemu mbalimbali

Nikaamua nichukue na vocha ya elfu 10 kwa nia ya kuniuunga kifurushi cha intaneti kisicho na kikomo cha wiki (Unlimited) kinachopatikana kwa Tsh 4999/=, pia nyingine nilijua nitatumia kwenye kifurushi cha maongezi.

Kosa nilililofanya nikaondoka na laini bila kuijaribu kwenye simu, nikijua simu yangu moja niliyokuwa nimeiacha kazini muda ule ndio ningeenda kuijaribia. Kufika kazini nagundua laini hiyo ni kubwa na simu yangu inaingiza laini za ukubwa mdogo (mini-simcard).

FUNDISHO
Kwako – Kama unadhani utatumia kwenye simu inayopokea kadi ndogo basi omba wakukatie kabisa unaponunua, sifahamu kama wana laini ndogo kabisa, ukienda jaribu kuulizia.
Kwa Halotel – Wakumbuke kuuliza wateja wanaenda kutumia kwenye simu za aina gani, ni rahisi sana kwa mteja kujisahau. Pili, kama inawezekana ziwepo zile zinazoweza kuvunjwa kirahisi kuweza kupata mini-simcard.

Nilivyofika kazini nilifanikiwa kuulizia kupitia mtandao wa Twitter kama kuna mtu anaweza nisaidia kupata sehemu ya kukata laini hiyo kwa eneo la posta. Nilipata majibu kutoka kwa marafiki kadhaa na nikabahatika kufika kwa mmoja na kufanikiwa kuikata.

SOMA PIA  Tanzania Kushirikiana na Toshiba katika Kuendeleza Nishati ya Jotoardhi

Nikiwa nimefurahi kwa mafanikio hayo na wakati huo nikawa nisharudi kazini – nikiwa nataka kuwaka vocha kuangalia mfukoni na kwenye begi, kote nikakuta patupu. Vocha yangu ya buku 10 kwa ajili ya kujaribia mtandao huo ikawa ishapotea. MAJANGA – Buku 10 nyingi….. 🙁

Siku ya Pili

Nilifanikiwa kufika tena kwenye duka lao la Victoria na nikafanikiwa kununua vocha tena, kutokana na sababu za kibajeti basi ikanibidi nichukue ya elfu 6 tuu kwa sasa.

Nilijiunga kifurushi cha intaneti bila kikomo cha 4,999/= na kwa 1,999/= nikajiunga kifurushi cha maongezi kupiga mitandao yote nchini – nilipata Dkk 30, SMS 300 na MB 60.

Intaneti yao ni ya kasi kweli, si kasi ya kimaajabu saaaaana ya kulinganishwa na mfumo wa 4G kutoka Smile. Ila ni kasi nzuri ya kuweza kukupa zaidi ya KB 150 kwa sekunde kwenye masuala ya Torrents/Download vitu kutoka mtandaoni. YouTube utaangalia Video bila shida yeyote.

Nilianza kuburudika a.k.a ku’enjoy’ kasi ya intaneti mara moja. Kipindi hicho nilikuwa posta mjini na nikasema labda kwa kuwa ni mjini lakini ata niliporudi nyumbani – mitaa ya kijitonyama bado huduma ya intaneti ilikuwa ya kasi na hakuna ata kialama kimoja cha ujazo wa mtandao kilikuwa kimeshuka na uwezo wa mtandao wa intaneti ulikuwa mara nyingi ni H+ na saa nyingine ukawa H tuu (Kufahamu tofauti za teknolojia za 3G tafadhali soma – Fahamu Tofauti Kuu Kati ya Teknolojia za 2G, 3G, 4G n.k )

SOMA PIA  Gari la Mitsubishi Outlander linaweza kudukuliwa kwa njia ya WiFi

Siku ya Tatu

Hii ilikuwa ni wikiendi – Jumamosi, nilifanikiwa kudhurura sehemu kadhaa na kote bado mtandao ulikuwa ni wa uhakika na kiwango cha huduma ya intaneti hakikuwa kimeshuka kabisa.

‘Siku ya tatu nikaugeuza simu yenye Halotel kuwa ndio simu ninayoitumia zaidi kwa huduma za intaneti nyumbani kwani nimekuwa nikihangaika kwa muda mrefu na gharama ghari za mtandao wa Smile kwani mitandao mingine yote huduma ya intaneti inakuwa mbovu sana eneo la ndani ya nyumba kwa maeneo ninayoishi. Kwa hiyo rasmi Halotel ikawa ndio laini ya simu ninayotumia zaidi’

Siku ya Nne

Jumapili – Siku ya Uchaguzi.

Niliendelea kufurahia huduma ya uhakika ya intaneti kutoka Halotel hadi wakati nipo kwenye mstari wa kusubiria foleni ya kupiga kura iliyochukua zaidi ya masaa manne nilikuwa bize Twitani nikijumuika na wengine katika kupata ‘updates’ (mirejesho) inayohusiana na yanayojiri katika vituo vingine vya upigaji kura. Nilifurahia intaneti ya uhakika kiasi cha kudodosha tweet kadhaa zinazohusu Halotel katika muda huo.

MAJANGAAAAAAAA YAKAJA

Baadae nikiwa nyumbani napitia pitia TeknoKona na kuweka mambo kadhaa sawa ghafla nikapata ujumbe mfupi (sms) ikinitaarifu nikwishatumia GB 1 na hivyo nitegemee kasi ya intaneti yangu kushuka kidogo. Nikasema hamna tatizo – ata ikishuka sikudhani kama itaathiri utumiaji mdogo mdogo.

Kitu kikakata!! – Yaap – Nilikuwa nafanya ‘tethering’ kwenye laptop na ghafla huduma ikawa sifuri, kurasa hazifunguki. Refresh wapiiiii. Nikaamia kwenye simu, nikafungua app ninayotumia muda mwingi zaidi, Twitter, nako pakawa patupu, kitu haki-load. Nikaona huu utani sasa. NIKAPIGA CUSTOMER CARE (HUDUMA KWA WATEJA – Namba 100)

Mhudumu aliwahi kupokea na nikaelezea tatizo langu, janga kubwa likajitokeza pia huyu mdada ata hakuwa anaelewa maana ya bando la intaneti la ‘unlimited’ yaani bila kikomo linafanyaje kazi, akawa ananiambia akiangalia kwenye akaunti yangu anaona MB zangu zimeisha. Ilichukua dakika kadhaa kuweka msimamo kuhusu bando ya UNLIMITED, akaniweka kusubiri na baadaye akasema nizime na kuwasha simu na huduma itarudi kama kawaida.

SOMA PIA  TWITTER: Mamia Ya Wafanyakazi Katika Hatihati Ya Kupoteza Kazi Zao!

Zima – washa -zima – washa, kitu wapi, nikaanza kupata huduma ila ikawa taratibu sana. Kumbuka sijahama kabisa, nipo eneo la nyumbani ambalo mwanzo nilikuwa nakula bata nono la intaneti ya kasi. Kutumia apps kama Twitter na Instagram itachukua muda kufungua baadhi ya picha, na kwenye mtandao ndio ikawa shida kabisa kufungua mitandao mbalimbali.

USHAURI WANGU

Labda bado mifumo ya vifurushi katika vifaa vyao bado haijakaa vizuri na hivyo kuwa na itilafu kadhaa. Kama ni hivyo basi Halotel wanatakiwa waliangalie hilo.

Pia mpaka Jumapili bado vocha zake upatikanaji wake haukuwa mzuri, sikufanikiwa kupata vocha. Duka moja waliniambia wanategemea kuwa nazo kuanzia Jumatano wiki hii. Hivyo hakikisha unaponunua laini basi hapo hapo chukua na vocha za kukutosha kwa kifurushi unachotaka tumia.

Cha pili, inawezekana ya kwamba waliposema spidi inakuwa ndogo baada ya GB kadhaa basi ndio inakuwa ndogo kweli kweli kiasi cha ata kutuma picha kwa WhatsApp au kuangalia picha ukiwa kwenye app ya Twitter inakuwa ni shida. Kama ni hivyo basi ni wajibu wao kuliangalia hili kwani linaondoa maana kubwa ya huduma ya UNLIMITED, kwa nini nilipie bando ambalo siwezi ata kutumia apps chache kwenye simu bila kuathiriwa na spidi ya intaneti kubaniwa?

Pia wahakikishe wahudumu walio kwenye ‘Call center’ wanaelewa kwa undani huduma zao zote. Inasikitisha kama mteja inabidi utumie dakika kadhaa kuweza kumuelewesha muhudumu maana ya kifurushi cha UNLIMITED.

Kwako, labdo tatizo hili limenitokea mimi tuu…unaweza ukajaribu kwako na kunipa maoni yako ila kama unataka kujiunga na bando la intaneti katika mtandao wa Halotel kwa sasa na kufurahia spidi ya kasi ya intaneti basi jiunge na kifurushu cha MB au GB kadhaa na si kifurushi cha UNLIMITED.

Kwa ujumla wake nimefuruhishwa sana kwa jinsi walivyohakikisha karibia sehemu nzima utakazozunguka hauwezi kukosa intaneti ya kasi kabisa ya H+, na uhakika mitandao mingine itabidi ihakikishe inasasisha (upgrade) mitambo yake yote haraka iwezekanavyo ili kuzidi kukaa kwenye ushindani. Vinginevyo Halotel itachukua wengi sana, na wakijaribu tuu wanaweza wakaufanya mtandao huo kuwa mtandao wao namba moja huku mingine ikisahaulika taratibu. 

Je na wewe umeujaribu mtandao huu? Niambie maoni yako. Nategemea makala itakuwa imekusaidia kufahamu na kujiandaa kama unafikiria kujiunga nao.

Comrade Mokiwa

Mbunifu na mpenda teknolojia.

Muanzilishi wa Teknokona, TechMsaada na Teknokona Group LTD - WWW.TEKNOKONAGROUP.COM

Muda wangu umegawanyika kati ya kazi kibunifu @teknokonagroup na uandishi wa habari za Teknolojia hapa Teknokona Blog.

| mhariri(at)teknokona.co.tz |

Comment

Comments

  1. […] post Uchambuzi: Nimetumia Halotel Kwa Siku Kadhaa, Fahamu Nilichokutana Nacho appeared first on […]

Leave a Reply

Your email address will not be published.

TeknoKona Teknolojia Tanzania