Ushawahi kusikia kuhusu kampuni ya Cellebrite kutoka nchini Israeli? Tusharepoti kuhusu kampuni hii na biashara waliyofanya na FBI, na sasa wamekuja na taarifa mpya. Wanamiliki teknolojia yenye uwezo wa kudukua simu yeyote inayotumia toleo la iOS 12.

Toleo la iOS 12 ndio toleo jipya zaidi kwenye simu za iPhone kwa sasa, na kampuni ya Cellebrite kutoka Israeli imesema inamiliki teknolojia ya kuiwezesha kudukua data za simu yeyote ya iPhone au kifaa cha iPad kinachotumia toleo hili.
Taarifa rasmi za Apple zinasema kuna takribani vifaa bilioni 1.4 vya Apple vinavyotumia toleo la iOS 12 kwa sasa duniani kote. Data za watu hawa wote kuwa katika hatari hii ni jambo la hatari kwa kampuni inayojisifia sana kwenye masuala ya usalama wa data za watumiaji wake.
Kampuni ya Cellebrite si kampuni ndogo katika masuala haya. Tayari mwaka 2016 inasemekana shirika la usalama na uchunguzi la Marekani la FBI liliwalipa ili kuweza kudukua data za simu ya iPhone 5c katika kesi iliyohusisha ugaidi – hii ni baada ya Apple kukataa kutoa ushirikiano wowote.
Ingawa kampuni hiyo inasema huwa inatoa ushirikiano kwa mashirika ya kiusalama tuu inasemekana tayari programu zake za udukuzi wa simu zishakutwa zikiuzwa kwenye mitandao kwa bei isiyozidi Tsh 250,000 ($100). Cellebrite wanajitetea wakisema teknolojia yao kutumika inahitaji mtu hadi awe na simu yako, na si kwa kutumia ukuzi wa mtandaoni.
Hichi ni kipindi ambacho tayari Apple wanajiandaa kutambulisha toleo la iOS 13, toleo ambalo simu za iPhone 5s, iPhone 6 na 6 Plus hazitaweza kulipata tena. Hii ina maanisha ata kama Apple ataweza kutatua tatizo kwenye toleo lijalo la iOS bado kuna mamilioni ya simu ambazo zitaendelea kubaki kwenye tatizo la uwezo wa kudukuliwa.
Chanzo: Forbes