Kampuni mashuhuri katika biashara ya programu inayotumika kuendesha kompyuta za aina mbalimbali duniani ya Microsoft wametambulisha rasmi toleo lililoiva la Windows 10.
Habari kubwa zaidi ni kwamba kama unatumia toleo la Windows 7 au 8/8.1 basi utaweza kushusha (download) na kupakua toleo la Windows 10 kupitia intaneti bure kabisa. Na ofa hii ni ya mwaka mmoja tu.
Kumbuka tulishaandika kwa undani sifa mbalimbali ambazo zilishatambulishwa mapema zaidi, soma hapa -> Microsoft Waruka Windows 9 na Kuja na Windows 10!, ila leo tutazitaja baadhi hizo kwa ufupi na pia tutakuambia mambo mapya ambayo hayakuwepo kwenye makala ya mwanza.
Kumbuka ata kama wewe ni mtumiaji wa simu janja inayotumia Windows 8 basi nawe pia utaweza kupata tolo la Windows 10 bure kabisa. Windows 7 bado inashika chati katika utumiaji, watafiti wengi wanasema uamuzi wa kuifanya bure kwa muda ni wa kuisaidia watu wengi kuhamia kwa haraka zaidi.
Hizi ni baadhi ya sifa za Windows 10 ambazo zimetengazwa masaa machache yaliyopita huko Marekani katika tukio liliandaliwa na Microsoft kuhusu Windows 10.
Cortana
Kwa watumiaji wa iPhone watakuwa wanatambua app maarufu ya Siri inayoweza kukusaidia kuwasiliana na simu yako, utaweza kuuliza maswali na ata kutafuta mafaili yako kwa kuongea na programu hii ya Cortana. Hii itarahisisha utafutaji wa mafaili na mambo mengine kwa wale waliowazito kutumia kipanya au kutumia kibodi zaidi.
Je ni jinsi gani utaweza kuitumia programu hii ya Cortana?
- Itaweza kufungua faili lolote utakalolitaka
- Itaweza kutafuta picha zilizopigwa tarehe flani
- Badala ya wewe kuandika barua pepe, utaiongea na programu hii itakuandikia na kuituma
- Itakupatia utabiri wa hali ya hewa na ushauri wa mavazi kulingana na hali hiyo
Kwaheri Internet Explorer, Karibu Spartan!
Windows 10 inakuja na programu mpya kwa ajili ya kutumia mtandao iitwayo Spartan. Ujio wa Chrome na Firefox uliharibu kabisa ukuaji wa Internet Explorer, kiasi ya kufikia hali ya kuilinganisha Internet Explorer na teknolojia ya kizamani zaidi. Microsoft wanataka kuanza upya na wanakuja na Spartan. Spartan itapatikana katika vifaa vyote vinavyotumia Windows 10 hii ikiwa ni kompyuta, tableti pamoja na simu janja.
Kitu kwa ajili ya watumiaji wa mfumo wa gemu wa XBOX (unamilikiwa na Microsoft)
Watumiaji wa gemu la XBOX wataweza kuhamishia na kuonesha michezo yao kwenye vioo vingine kama vile vya tableti, simu au kompyuta zinazotumia Windows 10. Inatakiwa tuu ziwe zinatumia mtandao mmoja wa WiFi na XBOX.
Programu za Excel, Word na PowerPoint kuja moja kwa moja kwenye simu na tableti!
Ndiyo, kwa wale watumiaji wa simu na tableti basi wataweza kupata apps hizo maarufu moja kwa moja bureee.
Je Start Menu imerudi?
Uwezo wa kuweka chaguo la kufanya muonekano wenye StartUp moja kwa moja kila kompyuta inapowashwa. Kumbuka muonekano huu ni ule uliozoeleka zaidi na uliondolewa na ujio wa Windows 8 na wengi walichukizwa na badiliko hilo.
Katika Windows 10 basi mtumiaji wa tableti au simu anaweza kuchagua muonekano kama ule wa WIndows 8, wa viboksi viboksi kwenye ‘menu’ kuwa mkuu wakati watumiaji wa kompyuta wataweza kuuondoa na kufanya ule muonekano wenye ‘Start Up menu’ kuwa ndio muonekano mkuu wanapowasha kompyuta yao.
Je nini Microsoft hawajakisema?
Hawajasema ni lini toleo hilo litatolewa rasmi kwa watu wote, kumbuka kwa sasa unaweza kutumia toleo lisilorasmi kwa ajili ya wote – Developer Technical Preview. Kama unakompyuta usiyoitumia kwa ajili ya kazi muhimu za kila siku basi unaweza itumia. (Bofya hapa Windows 10 Developer Preview kujua jinsi ya kutumia toleo hilo)
Soma sifa hizi na zingine kwa undani katika makala yetu nyingine hapa -> Microsoft Waruka Windows 9 na Kuja na Windows 10
Endelea kusoma TeknoKona,!
Twitter – www.twitter.com/teknokona
Facebook – www.facebook.com/teknokona
Instagram – www.instagram.com/teknokona
No Comment! Be the first one.