Simu feki za android zipo madukani kwa wingi na tayari zimejipatia jina maarufu la ”kloni”. Itakushtua zaidi kwamba simu hizi zinafanana sana na orijino na si rahisi sana kuzigundua kwa haraka.
Kloni zimekuwa gumzo sana kwa Android kwa sababu, tofauti na mifumo endeshaji mingine, Android haimilikiwi na mtu au taasisi yoyote bali, inalelewa na Google. Kwa sababu hii, kampuni yoyote inaweza kuitumia itakavyo na kwa minajili hiyo, wafanyabiashara waovu huitumia kuwarubuni watu wengine.
Ufanye nini kubaini simu halisi?
Kubaini simu halisi si jambo rahisi. Jambo hili linategemea sana muda na uerevu wako, hata-hivyo, kuna njia chache za kukusaidia kuibaini simu halisi ya Android:
1. Angalia kwa makini jinsi simu ilivyotengenezwa kwa nje
Simu feki hujulikana kirahisi ukiangalia jinsi vibonyezo (batani) zilivyotengenezwa. Kloni huwa na batani zilizolegea na umakini wa kutengeneza simu nzima huwa mdogo sana. Unaweza kuangalia pia jinsi jina la simu husika lilivyoandikwa, kamera, ‘sensor’, umbali wa skrini kutoka pembezoni na mwanga wa skrini ya simu. Hizi huonekana tofauti sana na zile za simu halisi na itakuwa vizuri ukibeba simu uliyo na uhakika nayo ili kutofautisha.
2. Tumia kamera na angalia spidi ya simu
Kitu cha pili muhimu kuangalia ni camera. Simu feki hujitangaza mapema kabisa kwa kamera yake. Picha ya simu feki haiwezi kuwa maridadi. Chunguza sana jambo hili. Lazima kuwepo na ukungu-ukungu utakaojionyesha. Ukimaliza hapo, shusha programu moja nzito kama Google Drive au Google Docs na angalia jinsi hiyo simu itakavyoimudu. Kama ni simu inayofanana na ya bei kali kama Samsung Galaxy S5, shusha gemu moja nzito na angalia jinsi itakavyoimudu pia. Kama simu itaonyesha kulegalega, basi ongeza mashaka.
3. Chunguza Uwezo wa simu
Unapopata simu ya Android, jaribu kuingia mtandaoni na kutafuta uwezo ( ‘phone specifications’ ) wa simu husika kwa ku-google kwa mfano, ‘Samsung S5 Specifications’. Ukishapata orodha ya uwezo wa simu husika, ingia kwenye settings na tafuta ‘Storage’ na pia angalia ‘About Phone/Device’ kwa ajili ya ‘model number’ na ‘build number.’ Hapa utaweza kuhakiki uhifadhi wa simu na pia namba ya modeli ya simu na pia build number ambayo unaweza kutafuta mtandaoni kama zinalingana. Ingawa simu nyingine zinaweza kudanganya uwezo, unaweza pia kushusha program mojawapo kama CPU / RAM / DEVICE Identifier kudhibitisha prosesa na kumbukumbu (RAM).
4. Tafuta ‘code’ maalum kwa simu husika
Watengenezaji wa simu wanajitahidi sana kulinda biashara yao na kwa maana hiyo huweka namba maalumu (‘service test codes au secret codes’) za kuhakiki uwezo wa simu yako kwa usalama zaidi. Namba hizo unaweza kuzipata ukichukua muda kidogo na kuchungulia mtandaoni.
5. Tumia programu ya kompyuta
Unaweza kuhakiki simu halisi kwa kutumia programu maalumu ya kampuni husika. Hizi programu zinapatikana kwenye kurasa rasmi za kampuni za simu kubwa duniani. Ukiunga simu kwenye kompyuta kwa kutumia USB, programu hizo zina uwezo wa kukupa modeli namba ya simu hiyo na taarifa nyingine muhimu kuhusu simu hiyo.
Ingawa elimu kidogo inaweza kukusaidia sana kuepukana na matapeli, kinga ni vyema zaidi kuliko matibabu. Hii ina maana kwamba, itakupendeza zaidi kama utajiwekea kanuni za msingi ili kamwe usipate mkasa wa kupoteza hela kwa simu feki. Kumbuka vitu hivi vya msingi sana:
Moja: Nunua simu kwenye duka linaloaminika.
Pili: Ikiwezekana, jaribu sana kununua simu kwa garantii ya muda mrefu.
Tatu: Epuka matapeli. Kama umepata dili linaloonekana kuwa zuri kupindukia, tumia njia hizi nne ulizopata hapa na kama bado hauna uhakika – achana nayo.
Kumbuka unaweza kuungana nasi kwa maswali na maoni kupitia akaunti zetu za Twitter, Facebook naInstagram .
Picha na www.phonesreview.co.uk
No Comment! Be the first one.