Mtandao wa simu wa TTCL umesema tayari wameanza kutekeleza mpango mrefu wa kusambaza huduma zao katika mfumo wa teknolojia ya kisasa zaidi ya 4G LTE.Awamu ya kwanza imeanza kwa kuweka minara 11 ya huduma ya 4G katika jiji la Dar es Salaam.
Kwa muda mrefu wengi wamekuwa wakiona mtandao huo wa simu ukiwa umelala na kutojitangaza kwa nguvu huku ukijisahau ya kwamba upo katika soko lenye ushindani mkubwa kutoka kwenye makampuni mengine.
Kuweza kusambaza huduma ya 4G LTE katika mkoa mzima wa Dar es Salaam pekee kutaitaji wawekeze katika takribani minara 266. Kwa sasa minara 11 waliyoanza nayo imewekwa katika maeneo ya kiwanja cha ndege cha JKIA, Barabara ya Pugu, eneo la makao makuu ya Posta (mjini), Upanga, Kinondoni, Ubungo, Oysterbay, Mwenge, Mbezi Tangibovu, Mbezi exchange, Kunduchi Salasala, Wazo Hill pamoja na Tegeta.
“Soma Pia – Fahamu Tofauti Kuu Kati ya Teknolojia za 2G, 3G, 4G n.k“
Kwa sasa imetumia mapato yake yenyewe katika kuanzisha huduma hiyo ila mtandao huo wa simu mkongwe nchini unategemea kupata pesa zaidi kutoka benki ya maendeleo ya TIB, kwa sasa wanasubiria kupata dhamana ya Serikali.
Mpango mzima wa usambazaji wa teknolojia hiyo ya 4G LTE unategemewa kuchukua miaka mitano.
Katika mpango wao wa muda mrefu wanategemea hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2016 watakuwa wameshafikisha huduma ya 4G LTE na baadhi ya sehemu 3G katika mikoa 10 zaidi na pia katika barabara zote kuu nchini. Mikoa inayotegemewa kuanza kufikiwa na huduma hiyo ni pamoja na Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, Tanga, Mtwara, Kilimanjaro, Iringa, Morogoro pamoja na Zanzibar.
Kwa kipindi kirefu wengi waliona kama vile shirika hilo limelala na linashindwa kutumia nafasi yake ya kipekee kama shirika la taifa kuweza kukua kwa kasi kama vile mitandao mingine isiyo ya kiserikali ilivyofanikiwa kufanya.
Ingawa wana huduma inayoridhisha bado kampuni hiyo ipo nyuma katika kujiuza na kuwashawishi watumiaji wengi wa huduma za intaneti na simu kujiunga nao. Soko la biashara ya mawasiliano imezidi kuwa ya upinzani zaidi baada ya kuongezeka kwa mitandao mingine miwili ya simu hivi karibuni, Smart na Halotel ambao wote wamewekeza pia sana kwenye huduma ya intaneti ya kasi.
Ni hatua nzuri kwa TTCL kuamua kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ya 4G LTE inayosifika kwa kuwa na kasi kubwa na ili waweze kufanikiwa zaidi. TeknoKona tunasubiria kwa hamu usambazaji mkubwa wa huduma hiyo na hakika tutaijaribu na kukutaarifu ubora wake.
No Comment! Be the first one.