Serikali ya Tanzania kupitia mashirika mbalimbali ya kimaendeleo inajihusisha na ufuatiliaji, usimamiaji pamoja na uendeshaji wa shughuli za TEHAMA. Mashirika mengi ya serikali yanayohusika na TEHAMA yapo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na mengine yapo chini ya wizara zingine.
Mashirika ya serikali yanayohusika na TEHAMA yaliyo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni pamoja na TCRA, TCRA-CCC, ICT Commission, UCSAF na TPC. Mashirika mengine yanayohusika na TEHAMA lakini hayapo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni kama TISPA na e-GA. Mashirika haya yana majukumu yafuatayo:
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA): Ni taasisi ya kiserikali yenye majukumu ya kusimamia sekta za Mawasiliano na Utangazaji Tanzania. Ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003 kusimamia huduma za kielektroniki na posta na masafa ya mawasiliano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. TCRA ilianza kazi tarehe 1 Novemba 2003.
Tume ya TEHAMA (ICTC): Tume ya TEHAMA ilianzishwa Novemba, 2015, Tume hii ilianzishwa kufuatia Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 iliyoidhinishwa na Serikali mwezi Machi 2003 ambayo ilielekeza kuanzishwa kwa chombo katika mfumo wa kitaasisi wa sekta hiyo ili kuratibu na kuwezesha sera. utekelezaji nchini. Lengo kuu la tume hii ni Kuongoza Jumuiya shirikishi ya Maarifa na Habari ikichangia ukuaji wa uchumi wa Taifa nchini Tanzania kwa kutoa ushauri wa kiufundi na kisera katika masuala ya maendeleo ya sekta na uwekezaji wa kimkakati kwa kukuza usambazaji salama wa TEHAMA na utambuzi wa taaluma.
Shirika la Posta Tanzania (TPC): Shirika hili lilianzishwa mwaka 1994 kwaajili ya kutoa huduma za posta nchi nzima. Majukumu yake ni pamoja na kutuma na kupokea mizigo ya aina mbalimbali ndani na nje ya nchi. Pia shirika hili limejihusisha na utengenezaji wa mifume ya TEHAMA kwaajili ya kurahisisha utoaji wake wa huduma kwa wananchi. Mifumo hiyo ya TEHAMA iliyotengenezwa nao ni pamoja na Smart Posta na Posta Tracking S.
Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA): Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019. Ni taasisi yenye mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma. Mamlaka ya serikali ya Mtandao ipo chini ya Ofisi ya Raisi Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF): UCSAF ilianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria ya Bunge ya mwaka 2006 kwa lengo la kupeleka na kufanikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi waishio katika maeneo machache ya mijini na maeneo mengi yaliyo mbali vijijini yasio na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma ya mawasiliano. Mwaka 2009 kanuni za kuhuisha Mfuko zilipitishwa na Mfuko kuanza kazi tarehe 1 Julai 2009. Mpaka sasa UCSAF imefanikiwa kusambaza huduma za mawasiliano maeneo mbalimbali nchini na pia mwezi uliopita walizindua minara mipya 42 iliyojengwa kwa ufadhili wa UCSAF.
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC): TCRA-CCC ni chombo kilichoundwa kisheria chini ya kifungu cha 37 cha sheria ya mamlaka ya mawasiliano na. 12 ya mwaka 2003 kwa madhumuni ya kulinda na kutetea maslahi na haki za mtumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano Tanzania katika nyanja za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Utangazaji, Posta, Vifurushi na Vipeto. Ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi TCRA-CCC ina wajumbe wasiopungua watano katika mikoa 15 nchini.
No Comment! Be the first one.