Wabunge nchini Ufaransa wamepitisha mswada wa sheria ambao utapiga marufuku matumizi ya simu rununu na tabiti katika shule za nchini humo hususani katika muda wa masomo.
Kwa mujibu wa mswada huo wanafunzi wa umri wa chini ya miaka 15 hawataruhusiwa kuwa na simu wala tabiti katika maeneo ya ndani ya shule au wazizime iwapo watakuwa nazo.
Viongozi ambao wanaunga mkono mswada huo wamesema sheria mpya itasaidia kuzuia ongezeko la simu mashuleni na kupunguza upotevu wa muda kwa wanafunzi kutazama picha badala ya kusoma na kujifunza masomo ya shuleni.

Kawaida wanafunzi nchini Ufaransa waliruhusiwa kuwa na simu shuleni lakini hawakuruhusiwa kuzitumia wakiwa darasani kitu ambacho wanafunzi wengi hawakuzingatia na badala yake walizitumia ndani ya madarasa yao.