Ukuaji wa teknolojia umegusa kila sekta ikiwemo sekta ya Kilimo. Teknolojia ya kilimo ni matumizi ya teknolojia katika kilimo ili kuboresha mavuno, ufanisi wa kazi pamoja na kuongeza faida. Kuna faida nyingi za kutumia teknolojia katika kilimo ikiwemo usimamiaji mzuri wa mashamba na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao.
Teknolojia zinazotumika katika kilimo ni pamoja na sensa za udongo, ndege isiyo na rubani (drone), Mfumo wa habari wa kijiografia (GIS), GPS, Mashine mbalimbali na Programu za kilimo. Terknolojia hizi zinatumika kama ifuatavyo;
Sensa za Udongo: Kuna vifaa mbalimbali vya kielektroniki ambavyo mkulima anaweza kutumia kupima hali ya udongo ya shamba lake. Vifaa hivi vya kielektroniki vinavyotumika huwa na sensa ambazo zinaweza kutambua hali ya unyevu iliyopo kwenye udongo, rutuba ya udongo pamoja na joto lililopo kwenye udongo. Kupitia taarifa zitakazo kusanywa na vifaa hivi vya kielektroniki mkulima anaweza kufahamu jinsi ya kuboresha uzalishaji wa mazao katika shamba lake.

Ndege isiyo na Rubani (Drone): Wakulima wenye mashamba makubwa hutumia ndege zisizo na rubani kukagua mashamba yao, kupulizia dawa katika mazao pamoja na kumwagilia mazao. Ndege hizi zimekuwa msaada sana kwa wakulima na zimesaidia kuongeza ufanisi katika upuliziaji wa dawa kwenye mashamba makubwa na pia kukagua na kutambua ni eneo lenye shida shambani ili mkulima aweze kulishughulikia mapema.

Mfumo wa Habari wa Kijiografia (GIS): Huu ni mfumo unaotumika kuchanganua taarifa katika aina mbalimbali za ramani. Kupitia taarifa zinaokusanywa katika mfumo huu mkulima anaweza kutabiri madhara ya hali ya hewa katika shamba lake na kujipanga nayo. Pia kupitia mfumo huu mkulima anaweza kufahamu ni kipindi kipi anaweza kulima au kuvuna shambani kwake.
Programu za Kilimo: Hizi ni programu maalumu kwaajili ya kusimamia shughuli za kilimo. Programu hizi zinaweza kutumika kupitia kompyuta au hata simu janja ambapo zitakuwa na uwezo wa kuwasiliana na sensa ulizoweka kwenye udongo na kukusanya pamoja na kuzihifadhi hizo taarifa pia zinamuwezesha mkulima kupanga ratiba ya shughuli mbalimbali za kufanyika shambani kila siku.
Mashine maalum za Kilimo: Mashine maalum za kilimo ni pamoja na matrekta ya kujiendesha yenyewe ambayo hutumika kwenye mashamba makubwa yanayopatikana nchi mbalimbali. Matrekta hayo hufanya shughuli mbalimbali kama kupanda, kuvuna, kupalilia na kuandaa shamba kwaajili ya kilimo. Mkulima anachotakiwa kufanya ni kutuma maelekezo kielektroniki ya kazi anayohitaji kufanyika na matrekta hayo.

No Comment! Be the first one.