Unazifahamu ndege kubwa kuliko zote duniani? Teknokona leo tunakuletea orodha ya Ndege zote kubwa duniani pamoja na taarifa zake kwa undani zaidi. Nchi zinazoongoza kwa utengenezaji wa ndege ni Marekani, Russia na China na mara nyingi huwa zinashirikiana katika utengenezaji na uundaji wa ndege hizi.
Ndege ya kwanza ilitengenezwa na kupaa mwaka 1903 nchini Marekani na tangu hapo teknolojia ya utengenezaji wa ndege iliendelea kukua na kupelekea mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Kuna makampuni mengi duniani yanayojihusisha na utengenezaji wa ndege ikiwemo kapuni ya Airbus, Boeing, Bombardier na Comac. Ndege kubwa kuliko zote duniani ni pamoja na:
Airbus A380: Hii ni ndege kubwa kuliko zote kwa upande wa ndege za kusafirisha abiria. Ndege hii ilitengenezwa na kampuni ya Airbus na kufanya majaribio yake ya kwanza mwaka 2005. Airbus A380 ina injini nne, ghorofa mbili, upana wa mabawa ni mita 80, urefu wake ni mita 73 na ina uwezo wa kubeba abiria 853. Mashirika ya ndege yanayotumia ndege hii ni pamoja na Emirates, Lufthansa, Singapore Airlines na mengine mengi.

Airbus Beluga: Hii ni ndege ya mizigo iliyotengenezwa na kampuni ya Airbus ili kurahisisha usafirishaji wa vipande na vifaa vya kutengenezea ndege vinavyotoka nchi zingine au kiwandani. Ndege hii ilitengenezwa mwaka 1994 na nchi zilizoshiriki katika utengenezaji wake ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Toleo jipya la aina hii ya ndege ni Airbus Beluga XL iliyotengenezwa mwaka 2014 na kupaa kwa mara ya kwanza mwaka 2020.

Antonov An-225: Hii ni ndege kubwa kuliko zote duniani kwa upande wa ndege za mizigo. Ndege hii ilitengenezwa mwaka 1988 nchini Ukrain kwa lengo la kusafirisha mizigo mikubwa na mizito. Inatumia injini sita na ina matairi 32, pia ndege hii ipo moja tu iliyotengenezwa. Antonov An-225 ina urefu wa mita 84, upana wa mabawa wa mita 88.4.

Boeing 747: Ndege hii ilishika rekodi ya kuwa ndege kubwa kuliko zote kwa kusafirisha abiria kwa miaka mingi kabla ya kutengenezwa kwa Airbus A380. Imetengenezwa na kampuni ya Boeing na imeanza kutumika tangu mwaka 1969 mpaka sasa. Kuna matoleo mbalimbali ya aina hii ya ndege yaliyofanyika mpaka kufikia mwaka 2021, matoleo hayo ni pamoja na Boeing 747SP, Boeing 747-400 na Boeing 747-8. Mashirika ya ndege yanayotumia ndege hii ni pamoja na Atlas Air na Lufthansa. Pia aina hii ya ndege imekuwa ikitumiwa na serikali za nchi mbalimbali ikiwemo Marekani kupitia toleo la Boeing VC-25 (Air Force One) na Boeing E-4. Boeing 747-8 ina uwezo wa kubeba abiria 467.

Endelea kutembelea tovuti yetu kujifunza zaidi kuhusu teknolojia mbalimbali na matumizi yake. Soma makala zetu zingine hapa.
Maelezo yanatujenga