Google wametangaza rasmi mambo mbalimbali ambayo tuyategemee kutoka kwao hili limetokea katika kongamano kubwa walilolifanya katika jiji la San Francisco huko Marekani masaa machache yaliyopita. Mambo yalikuwa mengi, kuanzia habari za toleo lijalo la Android, masuala ya malipo kwa simu, n.k. TeknoKona tumefuatilia kwa undani na sasa nawe pata kufahamu vyote muhimu vilivyojiri katika tukio hilo.
Android M: Toleo lijalo baada ya Android 5 – Lollipop
Android M ndio jina la sasa linalotumika kuongelea toleo lijalo la programu endeshaji ya Android baada ya hii ya sasa, Android Lollipop. Ni utamaduni wa Google kuficha jina rasmi la matoleo ya Android wanapoyatambulisha mwanzoni, huwa wanatumia herufi ya kwanza tuu na jina zima hutambulika baadae.
Katika tukio hili Google wametambulisha sifa mbalimbali za kipekee za toleo lijalo la Android. Kuna mambo mbalimbali ya kiupekee kama vile uwezo wa kupunguza utumiaji wa chaji kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na toleo la sasa la Android. Kusoma zaidi kuhusu Android M bofya Hapa – Fahamu Android M, Toleo Lijalo la Android
Android Pay
Kampuni ya Google tayari imekuwa na huduma ya malipo ifahamikayo kwa jina la Google Wallet, huduma ya Google Wallet itaendelea kuwepo ila nayo itakuwa sehemu ya moja tuu ya huduma kubwa zaidi ya malipo kwa kutumia simu ya mkononi waliyoitambulisha kwa jina la Android Pay. Huduma hiyo tayari imeshakubalika na makampuni mbalimbali ya uuzaji wa bidhaa na maduka makubwa nchini Marekani na hivyo itaweza kuanza kutumika mara moja ikianza rasmi. Kwa kiasi kikubwa uamuzi huu unaonekana ni wa kuzidi kuhakikisha hawaachwi nyuma na huduma ya malipo ya mpinzani mkubwa, Apple kupitia huduma ya Apple Pay.
Watumiaji wa Google Pay wataweza kubofya kwenye simu janja zao tuu na kufanya malipo bila kutoa pesa kwa waleti wala kutoa kadi zao za benki.
Huduma ya Apple Pay itakuwa inapatikana katika toleo la Android M lakini itasambaa hadi kwa Android KitKat.
Google Photos
Huduma za kuhifadhi, kuboresha na kufanya mabadiliko ya kimuonekano wa picha za ukubwa mbalimbali imeanzishwa na kupewa jina la Google Photos. Huduma hii itaanza kupatikana mara moja na Google wamesema tutarajie kuona apps za Google Photos kupitia soko la Google Play na la App Store kwa iOS. Huduma itakuwa inafanana na ile watumiaji wa Google Plus wamekuwa wakiitumia ila ni bora zaidi na uhifadhi wa picha zako online utakuwa bure kabisa, utaweza kuweka picha nyingi uwezavyo bila kizuizi cha ujazo.
Huduma hii itakuwa kwa ajili ya picha na video.
Google Maps kupatikana bila intaneti!
Huduma maarufu ya ramani ya Google Maps itapewa uwezo wa kuhifadhi data na kutumika ata pale ambapo unakuwa hauna intaneti. Pia ata pale itakapokuwa inakuelekeza njia itaweza kutoa maelekezo kutumia sauti bila ata ya intaneti. Kumbuka itaitaji uwe ushawahi kuitumia tumia ikiwa kwenye intaneti ili iweze kuzipata data za kiramani kwa ajili ya kutumika ata pale ambapo hauna huduma ya intaneti.
Pia wamesema uwezo huu utaweza kuja kupitia huduma za YouTube na kivinjari cha Chrome pia. Endelea kutembelea TeknoKona na tutakujulisha haya yakitokea.
Android Wear kwa ajili ya saa za mkononi za Android yapata maboresho.
Google wamesema watazidi kuboresha programu endeshaji ndogo ya Android kwa ajili ya saa (Android Wear), tayari programu endeshaji hiyo ina apps zaidi ya 4,000 ukilinganisha na apps zaidi ya 3,000 kwa programu endeshaji inayotumika kwenye saa za Apple.
Kuboresha Matangazo ya Mitandaoni
Katika hatua ambayo imeonekana ni ya kujitahidi kuleta ushindani katika eneo ambalo Facebook wanafanya vizuri kampuni ya Google imesema itafanya maboresho mbalimbali ya kuongeza uwezo mbalimbali wa katika huduma ya matangazo. Kama unatumia mtandao wa Facebook utakuwa unafahamu kuna matangazo ya aina mbalimbali kama vile yanayokuambia kabisa upakue app (install) na kuna yanayokuambia ununue bidhaa (buy) n.k, Google wamesema wanafanya maboresho na watangazaji wa matangazo wategemee kuona uwezo wa haya yote. Na zaidi katika hali inayoonekana kujaribu kuwavutia watengenezaji apps zaidi Google watawezesha ata matangazo ya apps kuweza kuonekana katika soko la Apps la Google Play.
No Comment! Be the first one.