App namba moja duniani kote kwa muda mrefu katika kutoa msaada wa wewe kuweza kujua taarifa mbalimbali kama jina la namba ngeni unazozipigia au unapopigiwa imekuwa TrueCaller, ila sasa kuna ushindani mkubwa umekuja.
Facebook wameleta app yao pia na lengo lake kiutendajiĀ ni kama vile TrueCaller, uitumie kama app ya kupiga na kupokea simu badala ya ile inayokuja moja kwa moja kwenye simu yako ya Android.
App hiyo kutoka Facebook inaitwa ‘Hello’ na tayari inapatikana katika soko la apps la Google Play. App hiyo inayofanya kazi za ‘Dialer’,(app ya kupiga na kupokea simu), itakuwa inatumia data mbalimbali kutoka kwa marafiki na wengine wengi kutoka kwenye mtandao wao wa Facebook.
Kazi zake hasa;
- Kutambua namba mpya kwa majina/ambazo hazipo kwenye namba ambazo tayari unazokwenye simu yako. (Data hizi zitatoka Facebook)
- Itakusaidia kuzuia, yaani ‘block’ namba ambazo utaki/upendi zikupigie
- Itakuwezesha kutafuta (search) namba za ofisi na mashirika ya kibiashara ya eneo lako
- Kama ukiwa unatumia intaneti kupitia teknolojia ya WiFi app hii itakuwezesha kupiga simu bila kutumia dakika/vocha za maongezi, itapiga kupitia mfumo wa intaneti (VoIP) yaani kama vile ambavyo WhatsApp inafanya kazi
- Kingine ni kwamba kama ukikuta simu ambayo hukupokea (Missed Call), kama aliyepiga yupo Facebook mara moja app hiyo itakupa uhuru wa kumjibu kupitia app yao ya kuchati ya Messenger
Afisa mmoja wa Facebook anayehusika na bidhaa/teknolojia zinazotengenezwa na kampuni hiyo amesema ya kwamba Facebook hawana mpango wa kutengeneza pesa kupitia app hiyo. Hii inamaanisha mambo mengi yatakayoweza fanyika kupitia app hiyo utayapata bure kabisa. Hili litaichanganya timu ya TrueCaller ambao bado baadhi ya maeneo katika app yao ni lazima mtu uwe umelipia.
Je TrueCaller wanatakiwa waogope?
Kwa kiasi flani kwani Facebook ni kampuni kubwa na watu wengi ambao tayari wapo Facebook wanaweza kuamua kujaribu app hii na kuipenda. Ila kwa upande mwingine wanaweza wasiwe na hofu sana kwani hii ni mara ya pili kwa Facebook kuja na app kwenye eneo la simu za Android. Walishakuja na app walioiita Home ambayo ilikuwa ni Launcher (app zinazobadilisha muonekano mzima wa simu za Android), haikupokelewa vizuri na watumiaji na hadi sasa inachukuliwa kama ni sehemu ambayo Facebook walishindwa kuvutia watumiaji. Labda ili linaweza tokea tena kwa app hii. Na sehemu ambayo TrueCaller itazidi kuwa inanguvu zaidi ya Facebook ni kwa kuwa TrueCaller inachukua data sehemu mbalimbali zaidi ya Facebook tuu.
No Comment! Be the first one.