Kupitia app ya Study, Facebook wanaomba data na watatoa malipo kwa wahusika wa data hizo. Je ni jambo ambalo unaweza kukubali kushiriki?
App hii ya Story ambayo itakuwa inafanya kazi masaa yote huku ikiangalia tabia za mtu na jinsi anavyotumia apps zingine mbalimbali kwa siku, data za mizunguko yake n.k. inategemewa kuanza kupatikana nchini Marekani na India hivi karibuni kabla ya kuanza kupatikana katika mataifa mengine, kwa watumiaji kwa njia ya mualiko.

Data kuu zitakazokuwa zinachukuliwa na app ya Study;
- Apps ambazo zimewekwa kwenye simu husika
- Muda unaotumia kwenye apps ulizonazo
- Nchi uliyopo
- Data kuhusu huduma gani unazitumia zaidi katika baadhi ya app ulizonazo
Facebook wamesema data kama vile ujumbe wa meseji katika apps za kuchati, nywila (passwords), na tovuti unazotembelea hazitarekodiwa.
App ya Study itapatikana kwa watumiaji wa umri wa miaka 18 na zaidi, na pia itakubidi ujaze fomu sehemu kuomba kuweza kuwa sehemu ya utafiti. Kigezo kingine cha kuweza kushiriki ni lazima uwe na akaunti ya PayPal kwa ajili ya kupokea malipo.
Hadi sasa Facebook hawajasema malipo yatakuwa ya kiasi gani. Kuhusu kuwa sehemu ya utafiti Facebook wamesema watawatumia walengwa matangazo ya kuwaomba kushiriki.