Uongozi wa Rais Trump umeiweka kampuni ya Xiaomi katika vikwazo vya kibiashara kwa kuiweka kwenye orodha ya makampuni na biashara ambazo watu na makampuni ya kimarekani hawaruhusiwi kuwekeza.
Orodha ya vikwazo hivyo ilikuja rasmi mwezi wa Novemba 2020, ikitaja marufuku kwa wananchi au makampuni ya kimarekani kuwekeza katika biashara au makampuni ya China ambayo yanadaiwa kuwa na mahusiano ya karibu na vyombo vya ulinzi na usalama vya China. Katika kipindi hicho Xiaomi haikuwepo kwenye orodha hiyo.

Katikati ya wiki kampuni hiyo ya Xiaomi imeingizwa rasmi katika orodha hiyo, mashirika ya kimarekani yenye hisa kwenye kampuni ya Xiaomi yanatakiwa kuondoa uwekezaji wao kufikia Novemba mwaka 2021.
Kumbuka Xiaomi inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa duniani kwa sasa kwenye biashara ya utengenezaji na uuzaji wa simu janja, nyuma ya Samsung na Apple. Imekuwa ikikua kwa kasi na imekuwa ni suala la muda tuu kabla ya kampuni hii kuipuka Apple.
Watafiti wengi wanaona kampuni ya Xiaomi imeonewa kuwa kwenye orodha hii. Nje ya simu na vifaa vingine kama TV n.k, Xiaomi haina vifaa vya mifumo ya kimawasiliano – ambavyo ndivyo vilivyoifanya Huawei kujikuta kwenye vikwazo vya Marekani.
Mwaka 2020 kampuni ya Xiaomi ilikuwa katika soko la hisa kwa zaidi ya asilimia 227 na kufikisha thamani ya dola bilioni 108 kufikia mwisho wa mwaka. Uamuzi huo wa Marekani umesababisha thamani kushuka na hadi Ijumaa ilikuwa imepoteza takribani dola bilioni 10 ya thamani.
Ni imani ya wengi kwamba kampuni ya Xiaomi inaweza ikaondolewa kwenye orodha hiyo na serikali mpya itakayoongozwa na Bwana Biden, ila nalo ni suala linaloweza kuwa gumu.
Je kuna tofauti ya vikwazo hivi na vile vya Huawei?
Ndio. Kwa sasa Xiaomi haijapigwa marufuku kutumia teknolojia za Marekani na hivyo itaendelea kutumia teknolojia nyingi muhimu ikiwa ni pamoja na zile za Google. Kwa sasa marufuku ni ya katika uwekezaji tuu.
No Comment! Be the first one.