Mmiliki wa Facebook Mark Zuckerberg yupo mbioni kufanya mchakato wa kuunganisha huduma za ujumbe wa mitandao maarufu ya kijamii ya Facebook, WhatsApp na Instagram kuweza kutuma ujumbe baina ya mitandao hiyo, imeripoti New York Times.
Mpango huo unaweza kuwa na faida kubwa kwa watumiaji mabilioni wa mitandao hiyo duniani kote kwa kuwarahisishia kutuma ujumbe kwenda kwa mtumiaji wa app nyingine kati ya hizo bila ya kulazimika kuwa na app hiyo nyingine kwenye simu yake kwa muda huo.

Watumiaji WhatsApp Facebook na Instagram wataweza kuwasiliana kwa urahisi. Kwa mfano mtu aliye na akaunti ya Facebook anaweza kumtumia ujumbe mtu aliye na akaunti ya WhatsApp tu.
Aidha Mark Zuckerberg amesema mitandao yote itatumia mfumo wa kiusalama maarufu wa ‘end to end encryption’ ili kuwepo na hali ya usalama na usiri kwa wanaowasiliana kupitia mitandao hiyo.
Mfumo wa end to end encryption ambao unatumika kwa WhatsApp kawaida mawasiliano yake yanaonwa na watu wawili tu wanaowasilina na si zaidi ya hapo.
Mpango wa uwezeshaji wa hilo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka 2020.
Mpango huo ni katika kuendelea kutoa huduma nzuri, bora wa kutuma ujumbe kwa haraka, rahisi na wa kuaminika zaidi. Ila si watu wote wamefurahishwa na jambo hili, wengine wanaona itakuwa ni njia rahisi kwa wadukuzi kufanikiwa kupata data za watumiaji wa app nyingine baada tuu ya kufanikiwa kudukua app nyingine.