Kuna wasomaji waliotaka kuifahamu simu ya Huawei Ascend Y530, wengine walitaka kuijua yenyewe kama yenyewe na wengine walitaka kufahamu tofauti yake na baadhi ya simu kutoka Tecno ambazo tushazielezea. Tutaielezea yenyewe kwa upekee wake ila kama utataka kulinganisha basi pitia makala zetu za nyuma za uchambuzi wa simu zingine kwa ajili ya ulinganishi wa kirahisi.
Simu ya Huawei Ascend Y530 ni simu janja iliyoingia sokoni katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2014. Simu hii ni ya kiwango cha kati kwenye eneo la simu janja, yaani kama unaitaji kununua simu janja na unabajeti ambayo haizidi laki mbili basi hii ni simu ambayo inaweza kukufaa.
Sifa zake kwa Ufupisho
- Kioo: Inchi 4.5
- Mawasiliano: Edge/2G/3G
- Kamera: MP 5 (Nyuma), MP 0.3 (Mbele).
- OS: Android, 4.3.
- Prosesa: Dual-Core, 1.2Ghz.
- Diski Uhifadhi: GB 4
- RAM: MB 512
- Betri: LI-ION1700 mAh.
- Rangi: Kuna nyeupe na nyeusi
Muonekano wake
Ina kioo cha inchi 4.5 (na ‘resolution ya 854×480) na ni cha mguso (touch screen). Nimepata nafasi ya kuichunguza kwa ukaribu simu hii wiki chache zilizopita katika duka moja jijini na ninaweza kusema kwa kulinganisha na bei yake simu hii inamuonekano mzuri wa nje. Nilipendezwa umbo lake la kona ndogo ilizonazo. Simu hii ina uzito wa takribani gramu 145, na usihofu inabebeka na kushikika vizuri kiganjani.
Ina wembamba wa milimita 9.3 na ninaweza kusema ni wembamba mzuri tuu unaoweza kumpendeza mtu yeyote asiyependa masimu manene manene 🙂
Programu Endeshaji
Simu hii inakuja ikiwa na toleo la Android 4.3 hivyo suala la upatikanaji wa apps si tatizo.
Kiufanisi;
Simu hii inakuja na RAM ya MB 512, hii ni kiwango cha kawaida ila kwa bei ya simu si jambo la kushangaza. Kwa utumiaji wa kawaida ni kiwango kinachotosha. Inakuja na kiwango cha ndani cha diski uhifadhi (storage) cha GB 4 na unapata nafasi ya kutumia SD memori kadi ya hadi ukubwa wa GB 32.
Kama ni mpenda kutumia apps zinazoitaji ufanisi mkubwa kama vile magemu simu hii inakuja na prosesa yenye ubora mzuri kulinganisha na bei yake. Inatumia prosesa ya 1.2 GHz Dual Core ( Snapdragon 200 MSM8210) ambayo kwa uchunguzi wa haraka haraka tuliofanya mtandaoni ni prosesa inayotosha kwa utumiaji usiomzito sana.
Vipi kwenye suala la Kamera?
Kamera yake ya nyuma ina lensi ya kawaida ya MegaPixels 5, wakati ye mbele kwa ajili selfi ni megapixels 0.3 tuu. Kwa kifupi huwa nasikitika sana nikiona viwango vibovu vinavyowekwaga kwenye kamera za mbele. Ila kwa simu zinazoangukia bei ya laki moja hadi mbili na nusu mara nyingi viwango vinakuwa ni hivi. Sikufanikiwa kuijaribisha na kuona tofauti yake kwenye kiwango cha picha hivyo sitaweza kuonesha hapa. Kingine ni kwamba kamera hiyo ya nyuma inauwezo wa ‘autofocus’ na ‘flash’.
Mawasiliano
Inauwezo wa EDGE/2G pamoja na 3G. Kwa wale wanaotumiaga simu zao kwa ajili ya kusambaza intaneti iwe kwenye mfumo wa ‘Tethering’ au ‘Wifi Hotspot’ pia wataweza kufanya hivyo.
Eeeh. Kuna redio pia. Utaweza kusikiliza radio katika mfumo wa FM.
Betri
Kiwango chake ni cha kawaida tuu, nacho ni 1700mAh, ila hichi ni cha juu kulinganisha na simu mbili za Tecno M3 na P3 tulizozichambua mara ya mwisho. Zile zote zinabetri la 1,400mAH. Ila si jambo la ajabu kwani simu hii inauwezo na bei kubwa zaidi ya hizo mbili. Kwa uwezo huu kama kawaida kwa simu janja nyingi usitegemee kutumia zaidi ya siku moja bila kulazimika kuchaji.
Bei
Uchunguzi wetu unaonesha sehemu nyingi hii ikiwa ni pamoja na maduka ya simu na maduka ndani ya ofisi za mitandao ya simu simu hii inauzwa kwa Tsh 195,000/=. Kutegemea na mahali ulipo bei haitakuwa tofauti sana na hii.
Je ushawahi kutumia simu ya Huawei? Tuambie mtazamo wako kuhusu ubora na uzuri wake. Na je ushawahi kutumia Huawei Ascend Y530? BOFYA eneo la kupiga kura utuambie.
[socialpoll id=”2265658″]
No Comment! Be the first one.