Wiki imeisha na habari ya Tigo kuleta teknolojia ya 4G kwa wateja wake wakianzia kwa mji wa Dar es Salaam. Hadi sasa mtandao namba moja katika teknolojia hiyo ni Smile Communications, hawa wamejikita katika kutoa huduma ya intaneti kwenye mfumo wa 4G pekee kwa maeneo ya Dar es Salaam, Arusha na tayari kuna taarifa ya kwamba wanajiandaa kusambaa sehemu nyingi zaidi.
Kwa sasa wakazi wa Masaki na maeneo yanayozunguka Mlimani City wataweza kupata 4G kutoka Tigo. Kufikia mwezi wa saba inategemewa maeneo mengine yote ya wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke yatakuwa yamefikiwa.
Je Tupo Tayari kwa Teknolojia ya 4G?
Hapa majibu ni ndiyo na ‘hapana-NDIYO’.
“Ndiyo” tunaitaji teknolojia hii kwa kuwa ni muhimu tusonge mbele kama nchi zingine kiteknolojia. Na kwa sasa teknolojia ya 4G ndiyo inayotumika kwa ajili ya kutoa huduma ya haraka zaidi katika masuala ya intaneti. Teknolojia ya 4G inahakikisha mtumiaji anapata uwezo wa kushusha (download) na kupandisha(upload) mafaili kwa kasi zaidi kulinganisha na mfumo wa 2G na 3G, kama umeshawahi kujaribu au kutumia mtandao wa Smile basi unafahamu tofauti kubwa iliyopo.
‘hapana-NDIYO’, “Hapana” haina nguvu kwa sababu maendeleo ni lazima na ni muhimu kwa eneo lolote lile na hasa kwenye eneo la teknolojia, ila kuna changamoto ambazo zipo na maboresho zaidi yasipofanyika haitaleta maana kuona tunakimbilia kwenye 4G wakati ata hiyo 3G bado ni tatizo.
Changamoto Zilizopo!
Kwanza kabisa kama ilivyo kwa vitu ambavyo ni vipya, teknolojia hii ni ghari sana katika kuweka na kuisimamia miundombinu yake (Hii ni sababu kubwa gharama za huduma kwa upande wa Smile ambao wanatoa huduma ya 4G pekee ni ghari sana). Na hakuna ubishi hadi sasa bei za data tumeona jinsi zilivyopandishwa kiajabu ajabu na kufanya watu kuogopa ata kupokea video kutoka kwa marafiki kwenye Whatsapp zao. Kama mwisho wa siku uamuzi huu hautawafanya kuongeza bei za gharama zilizopo basi ni jambo jema...ila kama gharama hizi zitawashukia watumiaji basi inawezekana habari mbaya zinaweza zikawa zipo njiani tena….
Kwa sasa kifurushi cha GB 5 kutoka kwa kampuni ya Smile wenye intaneti ya kasi sana kupitia teknolojia hii kinauzwa kwa takribani Tsh 42,500/=
Ya pili ni kwamba si kila aina ya simu au tableti inakubali kupokea ‘signal’ za 4G. Nachomaanisha hapa unaweza ukawa ni mtumiaji wa mtandao wa Tigo na umefurahia kwa sana kusikia kuna teknolojia mpya yenye spidi zaidi ikiwa inakuja bila kujua ya kwamba itakubidi nawe pia ununue simu yenye kukubali teknolojia hii, ambazo ni za bei ghari.Kwa kifupi jiandae kununua simu janja mpya, ni wachache tuu wanaomiliki simu janja za hali ya juu ambazo zinakuja tayari zikiwa na teknolojia hiyo ndani yake ndio wataweza kutumia 2G,3G, pamoja na 4G kwa kwenda eneo la ‘settings’ la simu zao. Pointi hapa ni kwamba bado wanufaikaji wa teknolojia watakuwa wachache sana, na nadhani kutokana na hili tumeona hata maeneo ambayo Tigo wanaanza nayo – Masaki na Mlimani City! Kama wewe unamipango ya kuonja hii 4G basi anza kujaza kibubu upate kununua simu janja yenye uwezo wa 4G! 🙂
Tatu, maeneo mengi mijini bado ata hiyo 3G kuipata ni tatizo!
Mimi naishi maeneo ya Kijitonyama, ofisi za kampuni ya Tigo zilizopo eneo hili zipo ukaribu wa kama kilomita 1-1.5 lakini intaneti inasumbua kwa sana tuu. Huu ni mfano tuu, kwani si kwa Tigo tuu bali ata kwa mitandao mingine bado kuna maeneo mbalimbali mijini kupata huduma ya intaneti yenye hadhi ya unacholipia ni shida sana. Kitu muhimu kwa sasa ingekuwa nikuhakikisha wanachowapatia wateja wake kimefikia kwenye ubora wa juu kabisa, baada ya hapo sasa ndio kufikiria kusogea mbele zaidi.
| Tayari Tigo walishatangaza kuwa na bajeti ya takribani Dola milioni 120 za kimarekani kwa ajili ya kuboresha huduma zao zaidi hasa kwenye eneo la intaneti hii ikiwa ni kusambaza teknolojia ya 3G pia, hivyo tunategemea mapungufu ya baadhi ya maeneo hii ikiwa ni pamoja na mijini kwenye matatizo yatatatuliwa |
No Comment! Be the first one.