Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA wametangaza kuja na kisimbusi kimoja kitakachoonyesha chaneli nyingi zaidi badala ya kuwa na kisimbusi (decorder) zaidi ya kimoja kuzipata zote.
Kisimbusi hicho kitakuwa na teknolojia ya cccam (card sharing) ambapo mtumiaji atakuwa anachomeka kadi maalum kupata chaneli anazokusudia badala ya kuwa na kisimbusi kingine.
Ni kwamba Kisimbusi hicho kitakuwa na uwezo wa kuingiza kadi maalumu itakayokupa fursa ya kupata Chaneli za aidha Azam, DSTV, Zuku, StarTimes, Digitek, Ting au Continental.
Mfano wake ni mtu kuwa na simu moja ambayo anaweza kuweka laini tofauti za kampuni za mawasiliano kupata huduma zao. Yaani kitakachokuwa kinabadilishwa ni cccam (card sharing) na sio Kisimbusi kama ilivyo sasa.
Mamlaka hiyo ya mawasiliano TCRA imeieleza kamati ya maendeleo ya kudumu ya Bunge kuja na mpango huo wa kuleta kisimbusi cha kuondoa kadhia ya kumiliki zaidi ya kisimbuzi kimoja.
Andrew Kisaka, mkuu wa kitengo cha leseni, amesema kwa kushirikiana na wadau wameweka utaratibu wa kuanza kuagiza Visimbuzi vya namna hiyo. Aidha amesema mtu yeyote anaweza kuagiza ila afuate utaratibu utakaowekwa.