Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekamilisha ujenzi wa kituo cha data ama Data centre ambacho ni kikubwa zaidi kwa Afrika Mashariki. Hii ni katika harakati za serikali kuhakikisha kwamba haibaki nyuma katika mbio za Tehama kwa nchi za Afrika mashariki.
Data centre hiyo ambayo ina miundombinu ya kisasa na madhubuti itakuwa inahost huduma za database kwa taasisi za serikali na pia taasisi za sekta binafsi. Hili litasaidia kushusha gharama za kufanya hudma hizo maana kwa sasa watu wengi wamekuwa waki zifuata huduma hizi huko ng’ambo.
Benki ya Exim ya China ilitoa msaada wa dola za kimarekani milioni 93.7 kwa ajiri ya kujengwa data centre tatu pamoja na kuendeleza mradi wa mkonga wa taifa wa fibre. Vituo vingine vitafungwa huko Zanzibar na Dodoma katika awamu zinazokuja.
Kituo cha data hiki kipo katika hatua za mwisho mwisho katika kuanza kazi na inategemewa pengine kitaanza kazi mwezi wa nne.
TTCL kwa niaba ya serikali ndio watakao kuwa wanasimamia mawasiliano katika kituo hiki, wakati Huawei wao ndio watakao hudumu kama washauri wakuu wa serikali juu ya masuala ya kiteknolojia katika kituo hiki.
Mpaka sasa kuna zaidi ya vijana mia moja wamepelekwa kwenda kusoma China ili kuwezesha serikali kuwa na nguvu kazi ya kutosha, na zaidi ya hayo wamekwisha kuja wataalamu mbalimbali kwa ajiri ya kuwafundisha wazawa.
Kituo hiki pia sio tuu kikubwa kwa Afrika Mashariki bali pia kinaendeshwa na umeme wa nguvu za jua, hii inafanya gharama za uendeshaji wa kituo hiki pindi kitakapoanza zisiwe kubwa sana.
Tunaendelea kufuatilia kama tutaweza kuyajua makampuni ambayo yataanza kukitumia kituo hiki,
Endelea kuwa na sisi kwa habari mbalimbali za teknolojia katika lugha yako tamu ya kiswahili.
Vyanzo: DataCenterDynamics, na mitandao mbalimbali