Je umeshaanza kugundua ya kwamba kuna simu nyingi siku hizi ata zinazotoka makampuni tofauti ya simu zinafanana muonekano? Je sababu ni nini?
Ni kwa sababu simu janja nyingi hazitengenezwi na makampuni tunayoyafahamu.
Asilimia kubwa ya simu janja zinazouzwa, kazi kubwa ya muonekano wake (design) na uwekaji wa vipuri vingine muhimu huwa inatengenezwa na makampuni ya viwanda makubwa matano ya nchini China. Makampuni yenye majina kama vile Xiaomi, Oppo, Huawei ata Samsung, kuna simu zao wanatengenezewa na viwanda hivi. Jambo hili limeanza kufanya simu nyingi kuanza kuwa na muonekano unaofanana – kwa sababu kinachobadilika ni jina la kampuni ya simu na sifa au uwezo wa simu unaotufautishwa na aina ya vipuri vinavyotumika ndani yake.
Kwenye biashara ya utengenezaji simu na ata bidhaa nyingine mbalimbali kwa ujumla kuna makundi mawili ya viwanda vya utengenezaji – kuna waofahamika kama OEMs na kuna wanaofahamika kama ODMs. Pia kuna mfumo mwingine wa tatu wa kibiashara na utengenezaji bidhaa unaofahamika kama OBM.


ODM – Original Design Manufacturing
Kwa kiswahili cha haraka hapa tunaweza sema âWatengenezaji Wabunifu wa Bidhaaâ. Hawa ni wale ambao wanafanya ubunifu wa bidhaa na kisha kuitengeneza. Mara nyingi pia wanaweza wakaboresha ubunifu wa bidhaa na kuwa na muonekano wa aina tofauti ya bidhaa ile ile moja.
>ODM kwenye Sekta ya Simu na vifaa vya elektroniki
Kwenye sekta ya simu viwanda/kampuni za mfumo wa ODM zinawekeza katika ubunifu mzima wa bidhaa. Kwa nchini China viwanda hivi vinaweza kutengeneza pia bidhaa hiyo katika muonekano mbalimbali wa kitofauti tofauti.
>Wanunuzi wakienda kwa Kiwanda cha ODM
Kampuni au mtu binafsi ambaye ni mfanyabiashara akienda kwenye kiwanda kinachotengeneza bidhaa kwa mfumo wa ODM basi atasema bidhaa anayohitaji, kisha kiwanda hicho kitampatia aina ya bidhaa hiyo ambazo zipo kwao. Mnunuaji atachugua aina ya bidhaa – mara nyingi tofauti ni muonekano na labda sifa zingine chache chache. Atalipia idadi anayohitaji, na atawapa logo ya kuwekwa kwenye bidhaa.
Baada ya hapo kiwanda hicho kitatengeneza bidhaa hizo na kupachika logo ya mnunuaji.

OEM – Original Equipment Manufacturing
Kwa kiswahili hawa tunaweza waita âWatengenezaji wa Bidhaa Kipekeeâ.
OEM wao hawafanyi kazi ya ubunifu, bali wanamtegemea mteja kuja na kazi nzima ya ubunifu na wao wanachofanya ni utengenezaji tuu kulingana na mahitaji ya mteja.
>OEM kwenye Sekta ya Simu na vifaa vya elektroniki
Mfano mkubwa hapa ni Apple, kampuni hii inatumia gharama zake mara zote kubuni na kutengeneza bidhaa mpya. Kisha baada ya hapo wanaipa kazi kampuni ya Foxconn ya nchini China kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa husika. Kila mwaka Apple wanafanya ubunifu mzima wa simu zao au laptop zao na kisha kazi ya utengenezaji inafanywa na Foxconn, Foxconn ni moja kati ya kampuni kubwa sana inayofanya kazi katika mfumo wa OEM.

>Mahusiano ya wanunuzi na kiwanda cha OEM
Mara nyingi wateja wao ni makampuni makubwa yanayowekeza pesa nyingi kwenye ubunifu. Katika teknolojia ya sasa bidhaa zinazoweza kuuzwa kwa bei nzuri ni zile ambazo zinabunifu katika kiwango cha juu, na hivyo ndio maana makampuni haya baada ya kutumia pesa nyingi kwenye ubunifu huenda kutafuta kampuni za mfumo wa OEM – kwa kuwa wanakuwa nao na mikataba mikali ya kulinda ubunifu wao.
Marekani ni moja ya taifa linalowekeza sana katika ubunifu wa bidhaa, ila utagundua bidhaa nyingi zinatengenezwa nchini China. China inaongeza kwa kuwa na viwanda vikubwa vya mifumo ya OEM – wateja wakiwa ni makampuni ya Marekani na mataifa mengi ambapo gharama za uendeshaji viwanda ni kubwa sana.
Ni vigumu mfanyabiashara mdogo, wa kununua na kuuza asiyefanya ubunifu wa bidhaa zake kuweza kufanya kazi na viwanda vya OEM.
OBM – Original Brand Manufacturing
Je inakuwaje pale kampuni inayofanya ubunifu, ndio inatengeneza pia bidhaa yake ndani ya viwanda vyake? Hivi ndio mfumo wa biashara ya OBM unavyoendeshwa. Kwa sasa mfano mkubwa ni kampuni ya Samsung, ingawa kuna simu kadhaa hasa za bei ya nafuu huwa zinatengenezwa kwenye mfumo wa biashara ya ODM, bado Samsung anatengeneza simu zake nyingi hasa za hadhi ya juu kupitia mfumo wa OBM.
Hali ilivyo kwa mwaka 2020
Data zinaonesha makampuni mengi ya simu yanaachia baadhi ya simu zake kutengenezwa na viwanda vya kwenye mfumo wa ODM. Ni kawaida kwa makampuni haya simu kutengeneza simu za hadhi ya juu kupitia viwanda vyake vya ndani au kupitia viwanda vya OEM, ila kwa simu za bei nafuu na hata za hadhi ya kati makampuni haya yameanza kuongeza kasi katika utumiaji wa viwanda vya ODM.

NA SASA MATOKEO YAKE YAMEANZA KUONEKANA – wanatumia viwanda vile vile vya ODM na hivyo tayari simu nyingi zimeanza kufanana kimuonekano ingawa zinatoka makmpuni ya ‘brand’ tofauti. Kwenye mfumo wa ODM katika biashara ya simu, kiwanda cha ODM kinapewa jukumu zima la ubunifu, na utengenezaji wa simu – kinachotoka kwa mteja/kampuni ya simu ni programu endeshaji tuu.
Je wewe umeanza kuliona hili? Leo utakuwa umegundua kwa nini hali hiyo inajitokeza. Tuambie mtazamo wako hapa au kupitia akaunti zetu za kijamii. Usisahau kushare na wengine. Facebook – @teknokona, Twitter – @teknokona, Instagram – @teknokona
Chanzo: Nokiamob na tovuti mbalimbali
No Comment! Be the first one.