LG kuacha kutengeneza simu janja – hiyo ni moja habari nzito katika wiki hii. LG ikiwa moja ya makampuni nguli kwenye teknolojia na moja ya makampuni ya kwanza kabisa kuanza kutengeneza simu janja zinazotumia Android.
LG ni moja ya kampuni iliyoingia kwa haraka sana kwenye biashara hii kwa mafanikio miaka mingi nyuma ila katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakipata ugumu kushika asilimia iletayo faida kwenye soko.
LG wamepoteza zaidi ya dola bilioni 4.5 (zaidi ya Tsh Trilioni 9) katika kipindi cha miaka mitano katika kuendesha biashara ya utengenezaji na uuzaji wa simu janja. LG ni kampuni kubwa Korea Kusini ikiwa na bidhaa nyingine nyingi kwenye sekta zingine na zikiendelea kufanya vizuri.


Katika memo iliyovuja kwenye vyombo vya habari Mkurugenzi wake Bwana Kwon Bong-seok amewataarifu wafanyakazi ya kwamba kuna uwezekano kampuni hiyo itafanya maamuzi ya kuachana na biashara hiyo kutokana na kutotengeneza faida yeyote kwenye biashara ya simu katika miaka mitano sasa.
LG wamekuwa wakijaribu kurudi vizuri kwenye soko kwa kuja na simu janja zenye vitu vya kuvutia nje ya vile vinavyopatikana kwenye simu nyingine – ila ingawa zinavutia ila zimeshindwa kushindana kwenye soko na simu zingine za hadhi ya juu kutoka Samsung na Huawei. Hivi karibuni wametambulisha simu zenye uwezo wa kuongeza skrini kupitia LG Wing na LG Rollable, simu hizi ni za ubunifu mkubwa na zinavutia lakini bado simu hizo hazijauzika vizuri.


LG wanafanya tathmini ya biashara yao ya simu janja ili kufanya uamuzi – uamuzi huo unaweza ukawa ni kuuza biashara yao ya simu janja, au kuifunga, au kupunguza ukubwa wa kitengo/idara ya biashara ya simu janja kwenye kampuni hiyo.
No Comment! Be the first one.