Kwa ufupi simu janja bilioni 1.43 ziliingizwa sokoni mwaka 2015, upo hapo? = 1,430,000,000 na hivyo kushikilia rekodi ya mwaka ambao uliingiza simu janja nyingi zaidi sokoni.
Ingawa tayari inaonekana manunuzi ya simu janja yameanza kupungua huku kampuni ya Apple ikionekana ndio inapata shida zaidi, data zinaonesha mwaka 2015 ndio unashikiria rekodi kwa utengenezaji na uingizaji sokoni wa simu janja nyingi zaidi.
Ukuaji wa asilimia 10
Ukilinganishwa na uingizaji wa simu janja sokoni kwa mwaka 2014, idadi hii ya simu janja bilioni 1.43 ni ukuaji wa asilimia 10. Data hizi zimetolewa na shirika la kimataifa la data – IDC (International Data Corporation).
Samsung bado kidedea, Apple na Huawei wakifuatia
Kampuni ya Samsung bado inashikilia nafasi ya juu kama kampuni iliyoingiza simu janja nyingi zaidi sokoni. Hii ikiwa na kuingiza idadi ya simu janja milioni 324.8 kwa mwaka huo huku katika idadi hiyo simu janja milioni 85.6 ziliingizwa katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka huo.
Samsung wanapata ushindani mkubwa katika soko la simu janja za ubora wa juu kutoka matoleo ya simu za iPhone kutoka Apple, huku katika eneo la simu janja za bei nafuu wanapata ushindani mkubwa kutoka kwa makampuni kama Huawei, Xiaomi, na Tecno kwa bara la Afrika.
Apple wanashika nafasi ya pili ingawa tayari wanategemea kutofanya vizuri sana kwa mwaka huu wa 2016. Wanashikiria nafasi ya pili huku wakiwa wameingiza idadi ya simu janja (iPhones) milioni 231.5, hii ikiwa ni ukuaji wa asilimia 20 ukilinganisha na mwaka 2014. Katika idadi hiyo iPhone milioni 74.8 ziliingizwa sokoni miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2015.
Katika makampuni ya simu yaliyofanya vizuri nje ya Samsung na Apple ni pamoja na Huawei. Kwa mara ya kwanza Huawei walifanikiwa kuingiza sokoni simu janja zaidi ya milioni 100 katika mwaka mmoja, ni makampuni machache tuu yashafanya hivyo hii ikiwa ni pamoja na Apple, Samsung, na Nokia.
Kwa mwaka 2015 Huawei waliingiza simu janja milioni 106.6 sokoni na katika hizo idadi ya simu janja milioni 32.4 ziliingizwa katika miezi mitatu ya mwisho ya mwaka huo.
Afisa wa shirika la IDC Bwana Melissa Chau anaamini Huawei ipo katika nafasi nzuri ya kuendelea kushika nafasi ya tatu kwa mwaka huu. Akiamini kampuni hiyo ya Uchina imefanikiwa kujitambulisha vizuri katika soko la dunia.
Muhimu: Data hizi zinahusisha idadi ya simu zilizotengenezwa na kuingia sokoni, na sio idadi kamili ya simu zilizouzika kwa wateja. Na pia haihusishi faida, kwani simu janja hizo zinatofautiana viwango, ubora na bei.
Je una maoni gani juu ya data hizi? Tuambie kwenye comment.
Chanzo: MYSinchew, IDC
No Comment! Be the first one.