Habari njema, kama wewe ni mtumiaji wa simu za Android basi hakikisha unaenda kwenye Google Play na kupakua toleo jipya zaidi la WhatsApp. Taarifa kutoka WhatsApp na kwa baadhi ya watumiaji wa app hiyo sehemu mbalimbali duniani zinasema tayari uwezo wa kupiga simu umeanza kupatikana kwa watumiaji wa app hiyo katika simu za Android.
Endelea kuhakikisha unapata toleo jipya zaidi, na utafahamu kama WhatsApp Call imewezeshwa kwa kuona mabadiliko ya kimuonekano hii ikiwa ni pamoja na kuona eneo la ‘Call’ likiwa sambamba na eneo la kuchati yaani ‘Chat’ pamoja na ‘Contacts’. Angalia kwa picha hii;
Je kwa watumiaji wa iPhone wataweza lini kupiga simu?
Timu ya WhatsApp wamesema watumiaji wa iOS yaani simu za iPhone itabidi wasubiri kidogo kwa takribani wiki kadhaa kuweza kupata toleo litakalowezesha upigaji wa simu.
Kilio kwa makampuni ya simu!
Makampuni ya mawasiliano ya simu yamechanganyikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na hili. Eneo la upigaji simu ndio eneo kubwa lililobakia linalowaingizia pesa. Ni kweli eneo la intaneti linaingiza mapato lakini si mengi na data kwa kiasi kikubwa ni bei rahisi ukilinganisha na gharama ya upigaji simu na hivyo makampuni mengi yameanza kuona WhatsApp kama inataka kuwaharibia biashara.
Fikiria kama marafiki na ndugu zako muhimu wote ukiwa na uwezo wa kuzungumza nao kupitia WhatsApp Call, hii itamaanisha utakuwa unajiunga huduma ya data tuu na kukimbia gharama kubwa za upigaji simu wa kawaida. Ni kweli tayari kumekuwa na apps za kuwezesha upigaji simu kupitia intaneti kama vile Viber na Skype, ila apps zote hizi hazijakuwa na watumiaji wengi sana kama vile WhatsApp (Zaidi ya milioni 700), ndio maana makampuni ya simu yana hofu.
Wakati makampuni ya simu yanakuna kichwa kutambua kama hili litaathiri kwa kiasi mapato yao wewe kama mtumiaji tambua habari njema kutoka WhatsApp ndio hii. Utaweza kupiga simu bure kabisa kupitia bando yako ya intaneti.
Gharama?
Ukiondoa kile kiwango cha kulipia WhatsApp baada ya mwaka mmoja wa bure cha dola 0.99 ya Marekani kwa mwaka inasemekana hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya gharama kutokana na ujio wa uwezo wa kupiga simu.
No Comment! Be the first one.