Ulimwengu wa sasa unategemea zaidi mawasiliano. Teknolojia nayo inabadilisha namna tunavyowasiliana. Watu wanahama kutoka njia za mawasiliano za kizamani na kufuata njia mpya za ki-intaneti zinazowapa uhuru zaidi wa kushirikishana hisia zao. Kampuni ya Rakuten, ya Japani imeendelea kufanya mapinduzi hayo ya mawasiliano na huduma yao ya meseji – Viber, ikiwa ni baada ya miezi michache tu tangu iinunue huduma hiyo kwa dola millioni 900 za kimarekani.
Sasa unaweza kumuangalia unayeongea nae kwa simu na Viber. Huduma hii inawezekana kwenye i-pad, i-phone na simu nyingine na tableti zenye mfumo-endeshaji wa Android 4.0, yani ‘Ice-cream Sandwich (ICS)’ au zaidi. Pia ni lazima unayeongea nae awe na kompyuta, simu au tableti ya namna hizo.
Kitu kinachovutia na cha kitofauti zaidi katika Viber ni uwezo wa kuhamisha maongezi
kutoka kwenye simu kwenda kwenye kompyuta na kuirudisha kwenye simuwakati maongezi yako hewani.
Muonekano wa Viber ni jambo kubwa ambalo pia Rakuten wamebadilisha. Viber imepata muonekano wa kisasa na wa kuvutia zaidi wa dizaini ya bapa – yani ‘flat design’, kwa lugha ya Malkia. Watumiaji kadhaa wa Viber watafurahi pia kujua kuwa hatimaye sasa wana uwezo wa kubadilishana namba kwa kutumia picha maalumu za ‘QR-codes’ kama vile ilivyozoeleka kwenye BBM.
Habari nyingine nzuri kutoka Rakuten ni kwa watu wanaotumia zaidi kompyuta kufanya kazi maofisini, shuleni au majumbani. Sasa watu hao watafurahia mawasiliano ya Viber kwenye kompyuta zao bila kuangalia kwenye simu. Faida ya hii ni kwamba huna haja ya kuinua simu kuwasiliana na watu kwa sauti au meseji wakati unafanya kazi, kitu ambacho kitakusaidia kuokoa muda wako. Viber inaweza kuwekwa kwenye kompyuta za Linux, Apple na pia kwenye simu, tableti na kompyuta za Windows.
Pamoja na vitu vingine, Viber pia inajiweka tofauti na huduma zingine za meseji kwa uwezo wa kutoa milio ya sauti (ku-mute) kwa mtu au kikundi kimoja-kimoja na uwepo wa soko la stika, amabazo zinazoongeza ladha ya mawasiliano ya meseji fupi. Rakuten wameeleza kuwa wanategemea kuongeza vitu vingine kwenye Viber kabla ya mwisho wa mwaka ikiwemo uwezo wa kufanya biashara kwa intaneti.
Unaweza kuipata Viber kupitia Google Play Store na usisite kutufikia hapa teknokona na kutupa maoni yako kwenye ukurasa wetu wa facebook kwa kubofya hapa na pia twitter kwa kubofya hapa.
No Comment! Be the first one.