Toleo jipya zaidi la Android ambalo lilianza kusambazwa mwezi Agosti tarehe 21 mwaka huu, bado halijasambaa katika vifaa vinavyotumia mfumo huu.

Mpaka sasa Oreo imeingia katika asilimia 0.5 ya vifaa vyote ambavyo vipo hai, hili ni ongezeko la asilimia 0.2 ukilinganisha na taarifa za mwezi uliopita.
Taarifa hizi zinaendelea kuthibitisha udhaifu wa mfumo mzima wa Android hasa ukilinganishwa na mfumo wa iOS ambao ndio mshindani mkubwa. Moja ya sifa za bidhaa za Apple ni kwamba kila wanapo toa toleo jipya la OS vifaa vingi husasisha OS zao kwenda matoleo mapya.
Je ni kwanini mfumo wa Android hausambai kwa kasi?
Android wanakutana na changamoto kutokana na ukweli kwamba mmiliki wa mfumo huu ambao ni Google hawajihusishi kutengeneza vifaa vingi vinavyotumia mfumo huu, watengenezaji wa vifaa kama Samsung, LG, Nokia, Tecno na wengine ndio wanayoidadi kubwa ya vifaa hivi.
Inawawia vigumu watengenezaji wa simu janja kuweza kuendeana na kasi ya Google ambao ndio watengenezaji wa Android, hii ni kutokana na ukweli kwamba kila kampuni ina vipaumbele vyake na zoezi zima la ku sasisha OS ya simu ni la gharama kubwa.
Ugumu kwa watengenezaji wa simu kusambaza matoleo mapya ya Android katika simu zao inatokana na ukweli kwamba kila toleo ni lazima makampuni yalirekebishe ili iweze kuendana na simu za kampuni husika na hapa ndio ambapo makampuni yanayotengeneza simu hushindwa kwa kuwa mchakato huchukua muda na pia ni gharama.
Pia makampuni mengine yanatumia suala hili kibiashara, ambapo wanaona ni bora matoleo mapya na mazuri ya Android kuyapeleka kwa simu zao mpya – ambapo mara nyingi zinakuwa za bei ya juu.
Je Google inafanya nini kuepuka hili?
Kwa sasa Google wanajaribu kuondoa hali hii kwa kuingia katika soko la utengenezaji wa simu ili waweze kufanya kama ambavyo Apple wamekuwa wakifanya, ila ni wazi itakuwa muda mrefu mpaka tuone simu za Android zikipata masasisho kwa wakati.