Jamani kilichokuwa hakitegemewi kutokea kimetokea! Kampuni ya Apple ambao ni watengenezaji wa simu za iPhones wamefanikiwa kuipita Samsung na kushika namba moja kimauzo kwenye soko la simu janja!
Data zilizotolewa na shirika la utafiti la Gartner limetoa data zinazoonesha katika kipindi cha robo tatu ya mwisho wa mwaka 2014 (Q4 – Mwezi wa 10-12) kampuni ya Apple ndiyo iliuza simu janja nyingi zaidi kuliko kampuni nyingine yeyote.
Mafanikio haya ya Apple yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mafanikio yake katika kukubalika na kuuzika kwa wingi kwa simu za iPhone 6 na iPhone 6 Plus.
[ Kufahamu zaidi kuhusu simu za iPhone 6 na 6 Plus bofya hapa – Apple waleta iPhone 6 & 6 Plus , Saa na Mfumo wa Malipo]
Kampuni | Q4 2014 – Mauzo(Mwezi 10-12) | Q4 2014 – % ktk Soko | Q3 2014 mauzo(Mwezi 7-9) | Q3 2014 – % ktk Soko | ||
Apple | m (Milioni) 74.8 | 20.4 | m. 50 | 17.8 | ||
Samsung | m. 73 | 19.9 | m. 83 | 29.5 | ||
Lenovo | m. 24 | 6.6 | m. 16 | 5.7 | ||
Huawei | m. 21 | 5.7 | m. 16 | 5.7 | ||
Xiaomi | m. 18.5 | 5.1 | m. 5.5 | 2 |
*Jedwali juu likionesha tofauti kati ya robo ya tatu na ya nne ya Mwaka 2014. Mauzo ni katika idadi za simu zilizouzika na si mapato ya pesa.
Ila kwa ujumla kwa mwaka jana wote ni Samsung ndio wanaoshika namba moja kimauzo, ila hii ni mara ya kwanza tokea mwaka 2011 wameweza kupokonywa namba moja katika mahesabu ya namna hii. Na kikubwa zaidi katika kampuni zote kubwa za juu ni Samsung pekee ndiye aliyeuza simu chache zaidi katika kipindi cha robo tatu hiyo ya mwisho, hivyo mafanikio ya kampuni ya Apple na wengine wengi yaliwafanya wapande juu zaidi.
Mafanikio ya iPhone 6 na 6 Plus zilizoingia sokoni mwezi wa tisa mwaka jana inaonesha ilikuza mauzo ya simu ya Apple kutoka milioni 50 zilizouzika katika kipindi cha robo tatu cha tatu (mwezi wa saba hadi wa tisa 2014) hadi karibia mara mbili, kwani katika kipindi cha robo ya mwisho wa mwaka huo waliuza zaidi ya simu milioni 74.8 wakati Samsung waliuza milioni 73, kutoka kuuza simu milioni 83 katika robo tatu iliyopita.
Kingine tunachoona ni pamoja na ukuaji unaoridhisha wa kampuni ya Huawei pamoja na Xiaomi. Wengi mtakuwa mnaifahamu kampuni ya Huawei kwani simu na modemu zao tayari zimekuwa nchini muda mrefu ila kwa ambao hawaifahamu Xiaomi – hii ni kampuni ambayo haina muda mrefu sana ambayo ilianzia kutengeneza simu kwa ajili ya soko la China tuu. Na baada ya mafanikio makubwa imeanza kusambaa, pia kumbuka kutokana na China kuwa pia na moja ya soko kubwa la simu kutokana na wingi wa watu katika taifa hilo mafanikio ya kampuni hii yanachangiwa na ilo pia.
Je unafikiri huu ndio utakuwa mwisho wa utawala wa Samsung katika namba 1 na nafasi hiyo kuchukuliwa na Apple moja kwa moja? Au simu mpya za Galaxy S6 na S6 Edge zinaweza hakikisha kampuni hiyo inarudi katika nafasi yake ya juu kabisa kwa mwaka huu labda? [Bofya kuzifahamu simu za Galaxy S6 na S6 Edge!]
Muda utatuambia! Endelea kusoma TeknoKona, kumbuka kusambaza maujanja na mahabari ya TeknoKona wengine pia wapate kufahamu! Ungana nasi pia kupitia Twitter, Facebook na Instagram
*Vyanzo – ZDnet na Gartner
No Comment! Be the first one.