Wakati dunia ikiusubiria kwa hamu mismu mpya wa ligi kuu ya mpira wa miguu Uingereza (almaarufu kama ‘Barclay’s Premier League’) uanze, timu maarufu ya Manchester United ilitangaza mapema wiki hii ilani ya kukataza vifaa vya kielektroniki (gajeti) vikubwa kama laptop na tableti kwenye mechi zao za nyumbani – ndani ya uwanja wao wa Old Trafford.
Timu hiyo kupitia barua pepe, imewaambia mashabiki wake kwamba uamuzi huo umechukuliwa kwa sababu za kiusalama. Barua hiyo imetaja hasa i-pad, inayotengenezwa na kampuni ya Apple kutoruhusiwa kabisa. Gajeti zingine zilizoingizwa kwenye orodha ya vitu visizyoruhusiwa Old Trafford ni zile zenye ukubwa wa 50mm x 100mm na juu.
Ilani hii imekuwa ikitumika nchini Uingereza kukataza gajeti zisizo na chaji kuingizwa kwenye ndege kubwa lakini timu hiyo ya United imetangaza kutoruhusu i-pad na gajeti zozote kubwa hata kama zina chaji. Wamesema hayo kwa sababu miundombinu ya uwanja haiwezi kutumika kiurahisi kutambua baina ya gajeti halali na zile za kigaidi zisizokuwa na chaji.
Hata hivyo, simu-janja na kamera zinaruhusiwa kama kawaida. Kwa sasa, United ndio timu pekee Uingereza yenye ilani hii huku wakisema kuwa ukubwa wa uwanja na umaarufu wake ndio unaofanya uwanja wa Old Trafford kuwa kwenye hatari.
Mpaka sasa, mashabiki wa Manchester United wameonekana kukubaliana na uamuzi huu mpya huku wengi wakisema kwamba tabia ya kutumia i-pad na gajeti nyingine inapunguza ladha ya ushabiki na raha ya mpira pale mtu akijaribu kuchukua video wakati mpira unaendelea.
Picha na Mashable Inc, whatmobile.net.
No Comment! Be the first one.