Umuhimu wa Tableti unazidi kuonekana duniani. Kila kukicha, mauzo ya gajeti hizi yanaongezeka. Ni dhahiri waatu wanahitaji kufanya kazi au kuburudika wakiwa njiani na vitumi vya mkononi.
Kwa kuona umuhimu huo, hii makala inakupa tableti tano bomba zinazopendwa na watu wengi na wachambuzi tofauti duniani mpaka sasa kwa mwaka huu.
5. Google Nexus 7
Tableti hii itumiayo mfumo-endeshaji wa Android inasifika kwa kuwa na uwezo mkubwa kwa bei poa ya kuanzia $332 (Tshs 551, 950). Nexus 7 ina kamera ya mbele tu ya megapixeli 1.2 itakayokuwezesha kuongea na watu uso-kwa-uso huku ukiweza kutumia mtandao kwa ‘wayalesi’ au 3G (kwa Nexus ya bei ya juu}. Tableti hii inauzwa katika ukubwa wa uhifadhi wa aina mbili – 16GB na 32GB . Ina kumbukumbu (RAM) ya 1GB na prosesa ya NVIDIA® Tegra® 3 quad-core kwa wale wanaolewa sayansi ya kompyuta zaidi. Vitu vingine ni microphone, mfumo wa Android 4.2 (‘Jelly Bean’) na betri ya kutosha masaa saba ya 4,325 mAh.
4. I-pad 2 (Yenye Retina Display)
Kampuni ya Apple inasifika kwa kutengeneza vitumi vya hali ya juu na dizaini inayovutia na I-pad 2 haiko mbali na sifa hizo. Hii ni tableti ya aina yake inayokuja katika aina mbili, I-pad 2 yenye wayalesi tu na yenye 3G. Ina urefu wa inchi 9.5 (241.2 mm), uzito wa takribani nusu kilo na nafasi ya kuanzia 16GB. Inabeba prosesa ya 1GHz dual-core Apple A5 inayokupa nguvu zaidi huku ikitumia umeme mdogo wa betrii kwenye skrini yenye muonekano wa kipekee wa Retina Display. Kwa matumizi ya kawaida ya I-pad hii, unaweza kutumia kwa masaa 6 na unaweza kujikombea kwa bei ya kuanzia $399 (Tshs 663, 337) ughaibuni.
3. Sony Xperia Z2
Sony wanaendelea kujitofautisha zaidi kwa kutengeneza vitumi vinavyohimili maji na Xperia Z2. Hii ni tableti kubwa (inchi 10), nyembamba, nyepesi (gramu 439) na iliyotengenezwa kwa muonekano wa kuvutia. Ina kasi kubwa ya kufanya kazi kwa prosesa ya 2.1 Ghz Quad-core na RAM ya 3GB ambazo kwa pamoja hufanya tableti hii kuwa ya kasi zaidi kwa ajili ya magemu na hata kufanya kazi maofisini kwa ushapu. Xperia Z2 inakuja kwa ukubwa wa uhifadhi wa 16GB na 32GB. Kitu ambacho kidogo hakiridhishi kwenye tableti hii ni uwezo wake wa kukaa na chaji ya betrii.
2. Samsung Galaxy Tab S
Samsung kwa sasa wanajulikana kwa kutengeneza vitumi vyenye uwezo wa kushangaza na zinakubalika bila kupiga mayowe. Galaxy Tab S ni mwendelezo wa disaini hiyo na ina vitu vingi sana kama uwezo wa kuingia kwenye Tableti yako kwa ku-‘scan’ kidole kama hupendi kuingiza namba au nywila, pamoja na uwezo wa kufanya mambo tofauti kwa wakati mmoja – kama kuangalia video huku ukifanya kazi nyingine.
Jambo lingine kutoka Samsung la kuvutia ni uwezo wa kuunganisha tableti hii na simu zake za hadhi ya juu, yani Galaxy S kwa ajili ya kupiga simu na kutuma meseji.
Galaxy Tab S ina kumbukumbu (RAM) yeneye 3GB, prosesa ya 1.3 na 1.9 Ghz ya Samasung Exyno 5 Octa na hifadhi ya 16GB. Ina kamera ya mbele ya megapixeli 2.1 na ya nyuma ya megapixeli 8 kwa picha maridadi zaidi.
Tableti hii ni ya hali ya juu na ambayo kwa sasa inashindanishwa na Xperia Z2 na I-pad Air tu. Dizaini yake ina ukubwa wa inchi 8.4 na 10.5 na uzito wa gramu 298 na 467.
1. I-pad Air
Hii ni tableti ya pili kwenye orodha hii kutoka kampuni ya Apple. Kitu kinachovutia kwenye I-pad Air kwanza ni disaini yake. Haitofautiani sana na I-pad mini yenye Retina Display, Apple wamechukua yale ya I-pad 2 na kuifanya I-pad Air kuwa nyepesi zaidi (gramu 469) na yenye mvuto zaidi.
I-pad Air ina skrini ya urefu wa inchi 9.7, yenye Retina Display kwa picha na video zenye muenekano bora. Ina uhifadhi wa kuanzia 16GB hadi 128GB, kumbukumbu ya 1GB na prosesa ya Apple A7. Kamera ya mbele, megapixeli 1.2 na ya nyuma 5MP. Kwa kutumia tableti hii unaweza kuunganishwa na intaneti kwa mtandao wa simu na wayalesi na betri yake unaweza kutumia hadi masaa 10 kwenye mtandao na wayalesi.
Kwa sasa, I-pad Air ndiyo inayotisha kutokana na mitandao mingi mikubwa duniani, ikishindana na Samsung na Sony Xperia kwa karibu kwenye ulimwengu wa tableti za hali ya juu. Hata hivyo kuna tableti nyingine ambazo hazijaonekana kwenye orodha hii ingawa ziko vizuri sana kama LG Pad 8.3, Amazon Kindle HDX7, Surface Pro 3 yenye mfumo wa Windows 8 na Samsung Galaxy Note Pro 8.4 na 12.2 ambazo unaweza kuzitazama pia.
Picha na tabletstats.com, samsung-updates.com, www.idownloadblog.com na www.pcadvisor.co.uk
Elimu nzuri xana
Asante sana Eliya