Je ushawahi kufahamu kuna tovuti inayokusaidia kuokoa mafaili yaliyodukuliwa inayokwenda kwa jina la No More Ransom? Tovuti hii ina programu mbalimbali za kusaidia kuokoa mafailia yaliyodukuliwa na kubadilishwa na kutoweza kutumika.
‘No More Ransom’ ni kimombo kinachomaanisha ‘Hakuna Tena Kulipa ili kuokoa kitu kilichotekwa’.
Tovuti ya No More Ransom inaendeshwa na kundi la washirika wengi linalohusisha vyombo vya kiusalama kama polisi na makampuni mbalimbali ya kiusalama wa kimtandao kama vile yanayotengeneza programu za ‘AntiVirus’ – kitengo cha usalama wa kidigitali cha bara la Ulaya – EUROPOL ndio kinasimamia mpango huo.

Kupitia umoja wao mashirika haya yanawekeza katika utengenezaji wa programu zinaweza kuokoa mafaili yanayodukuliwa na programu zilizotengenezwa na wadukuzi mbalimbali.
- Kikawaida programu hizi ukizishusha mtandaoni kimakosa (download) na kisha kupakua kwenye kompyuta yako unaweza kuta mafaili yakabadilika mfumo na kuwa katika mfumo usioeleweka wala kufanya kazi.
- Utashindwa kufuta wala kufanya chochote kuyaokoa mafaili hayo.
- Pia kunakuwa na ujumbe utakaokwambia kompyuta yako na mafaili yote yamedukuliwa, kama unataka kuweza kuyatumia tena basi utatakiwa ufanye malipo ya kipesa kwenda kwenye akaunti flani – siku hizi wadukuzi wengi wanataka ufanye malipo kwa njia ya BitCoin na kisha uwatumia barua pepe ya kuthibitisha kufanya hivyo – baada ya hapo ndio wataweza kukutumia neno siri litakaloweza kuyarudisha mafaili yako katika mfumo wa kutumika tena.
Udukuzi wa namna huu ni maarufu sana duniani na unawasababishia watu na makampuni mengi hasara nyingi kila mwaka. Katika kuokoa hili ndipo watu kadhaa na polisi wa nchini Ujerumani waliungana katika kuanzisha huduma ya kuwekeza katika programu za bure kwa ajili ya kuokoa mafaili yanayodukuliwa katika mfumo huu – hii ilikuwa Julai mwaka 2016.
Hadi sasa kuna jumla ya zaidi ya programu 82 ambazo zina uwezo wa kufungua mafaili ya teknolojia zaidi ya 109 za udukuzi. Programu hizi zimetengenezwa na makampuni mengi, kama vile BitDefender, Avast, Emsisoft, McCaffee na makampuni mengine mengi.
Ukijikuta katika shida ya namna hii na ukaona mafaili yako yamekataa kufanya kazi kazi jambo la kwanza kufanya ni kufahamu aina ya mdukuzi aliyehusika na kuona mafaili yako yamebadilika kwenda mfumo gani.
Ukifahamu hivyo basi unaenda kwenye tovuti ya No More Ransom na kuangalia programu husika kwa ajili ya udukuzi wa namna hiyo.
Inasemekana hadi sasa tovuti hii imesaidia kuokoa mabilioni ya pesa – hii ni kwa kuepusha watu au makampuni kuwalipa wadukuzi ili kuokea data zao. Na kumbuka matatizo haya si kwa kompyuta pekee, inaweza ikawa ata kwa simu.