Apple imezoea sana kushitaki makampuni mengine kama vile Samsung kwa muda mrefu ingawa kwa sasa inaonekana mahusiano yao yanachukua sura mpya ya ushirikiano zaidi…na sasa ni wao wanajikuta wakiburuzwa mahakamani na tena wakiwa na uwezekano mkubwa wa kujikuta wakilipa pesa nyingi sana.
Kampuni maarufu ya Erricson ya barani ulaya imeipeleka kampuni ya Apple mahakamani katika nchi tatu tofauti kwa wakati mmoja. Erricson imefungua kesi nchini Ujerumani, Uingereza pamoja na Uholanzi, katika kesi hizo kampuni hiyo inadai fidia za utumiaji wa baadhi ya teknolojia zake katika maeneo ya 2G na 4G zinazotumiwa katika vifaa vya kampuni ya Apple kama vile iPhone, iPads n.k bila wao kulipwa chochote.
Kesi hiyo pia inaangalia maeneo ya ubunifu wa vifaa mbalimbali vya elektroniki vinavyotumiwa katika utengenezaji na ufanyaji kazi wa simu. Kampuni ya Ericsson inaitaka kampuni ya Apple kuingia katika mkataba wa malipo ambapo Apple itakuwa inailipa fidia ya kiasi flani kwa kila wanapotumia teknolojia hizo katika vitu vyake.
Mwaka 2013 Samsung waliilipa kampuni ya Ericsson zaidi ya bilioni moja ya kitanzania kama malipo ya haki ya utumiaji wa teknolojia zake katika simu zake.
Ericsson ni moja ya makampuni ya mwanzo kabisa katika teknolojia za mawasiliano na kipindi flani ata wao walikuwa na biashara ya utengenezaji wa simu. Kwa sasa wamejikita katika biashara ya mitambo mikubwa ya mawasiliano na pia baadhi ya mapato yao makubwa yanatoka kwenye leseni ya kuyapa makampuni mengine ya utengenezaji simu kutumia baadhi ya teknolojia zake katika utengenezaji wa simu. Ericsson kama vile Nokia wanamiliki hakimiliki ya teknolojia nyingi za simu kwani walikuwa wa kwanza kabisa kujitosa katika ugunduzi wa teknolojia hizo miaka ya nyuma sana.
Inasemekana muda si mrefu kuna uwezekano mkubwa wa Ericsson kuwa wanapata mapato ya mabilioni ya shillingi kila mwaka kutoka Apple. Katika kesi hizi uwezekano wa Ericsson ni mkubwa kwani jambo hili lipo wazi kabisa ya kwamba Apple kama vile makampuni mengine yanayotumia teknolojia ambazo si zake ni wajibu wao kulipa baadhi ya mapato yao wanayopata kutokana na utumiaji huo.
No Comment! Be the first one.