Hivi karibuni zilisambaa taarifa kwamba simu feki zote nchini Tanzania zitazimwa ifikapo mwezi Juni mwaka 2016, makala hii itakuonesha jinsi ya kuangalia kama simu yako ni feki ama la.
Hatukuweza kuthibisha moja kwa moja kwamba kweli simu zitazimwa mwezi Juni lakini tumejiridhisha kuwa kutakuwa na hatua dhidi ya wanaomiliki simu feki pindi itakapofika tarehe hiyo.
Zifuatazo ni hatua unazoweza kuzitumia kuangalia kama simu yako ni fake, hakuna mahitaji makubwa kufanya hili ila tu unahitaji simu yako unayoitumia na unayotaka kuiangalia.
Jinsi ya angalia IMEI namba
- Andika *#06# kisha bonyeza kitufe cha kupiga
- Baada ya hapo simu yako itakuletea IMEI namba ambapo kama simu yako au kifaa chako kina laini mbili basi kutakuwa na IMEI namba mbili
- Namba hii pia unaweza kuipata katika boksi la simu ama nyuma ya ya simu hiyo baada ya kutoa betri, utaijua kwa kuwa huwa ni tarakimu 15.
- Nakili namba hizo pembeni.
Jinsi ya kuangalia kifaa kama ni feki ama halali
- Iandike ile namba uliyo nakili katika hatua iliyopita katika sehemu ya kuandikia ujumbe (SMS)
- Utume ujumbe huo kwenda namba 15090
- Baada ya kutuma meseji hiyo utaangaliziwa je hiyo IMEI namba ni ya simu ya aina gani na nani mtengenezaji wa simu hiyo.
- Subiri majibu (haitachukua muda mrefu)
- Ujumbe huo ukija unakuwa na maelezo ya kampuni iliyotengeneza simu hiyo pamoja na jina la simu hiyo.
Jinsi ya kujua kama simu yako ni feki
Kama jina la mtengenezaji wa simu yako pamoja na aina ya simu yako (Uliyo jibiwa baada ya kutuma IMEI namba) haviendani na majina ya simu yako (ambayo yameandikwa katika simu yako) basi ujue simu yako inamashaka na ni vyema kumuuliza muuzaji wako juu ya hilo.
Kama majina yaliyorudi hayaendani na majina yaliyoandikwa katika simu yako basi upo katika kundi lenye uwezekano wa kuwa na matatizo, TUNAKUSHAURI ufuate utaratibu na kuibadilisha ama kuacha kuitumia simu hiyo kabla ya mwezi Juni.
Kwanini TCRA wanataka tubadilishe simu
Simu isiyo na IMEI ni sawa na gari lisilo na namba za usajili {plate number}
Vyombo vya usalama vinaweza kukamata wahalifu wa kutumia mitandao ya simu kwa msaada wa IMEI namba hivyo mtu akiwa anatumia simu ambayo haina au ina IMEI namba ambayo sio sahihi anazuia utendaji kazi wa taasisi za usalama hivyo wao kama mamlaka wanatakiwa kuhakikisha kila mtu anatumia simu yenye IMEI namba sahihi.
Undelea kufuatilia Teknokona kwa habari mbalimbali katika lugha yako ya kiswahili.
4 Comments