Kampuni kubwa ya teknolojia duniani, Google Inc. imetangaza kufanikiwa kutengeneza gari linalojiendesha lisilohitaji dereva kabisa.
Gari hili lenye umbo dogo na spidi isiyozidi kilomita 40 kwa saa, limeripotiwa kuwa bila usukani, breki wala pakukanyagia mafuta na badala yake hutegemea teknolojia ya ramani ndani yake na ile ya mtandao, hutegemea kamera na vifaa maalum ‘sensors’ za kuhisi vitu vingine karibu yake.
Hii siyo mara ya kwanza google ya google kutengeneza gari linalojiendesha ila hili ni la kipekee kwa kuwa haliihitaji kabisa dereva wakati wowote. Awali, google ilitangaza nia ya kuwa kinara katika kuvumbua gari aina hii tangu mwaka 2010 kwa nia ya kupunguza vifo vya ajali za barabarani, athari za mazingira unaotokana na magari yatumiayo mafuta na adha ya usafiri mijini.
Google imefikia mbali katika teknolojia hii ila bado kuna changamoto nyingi ikiwemo kasi ya teknolojia kukua zaidi ya uwezo wa sheria za barabarani kuyabana magari haya mapya. Kwa sasa, Google imeweza kushawishi majimbo manne ya Marekani kuwaruhusu kufanya majaribio ya barabarani ili kujua jinsi gani yataweza kumudu utumikaji kwa walimwengu.
Teknolojia hii ya magari yanayojiendesha inafuatiliwa na watu wengi duniani pamoja na makampuni makubwa ya magari na teknolojia na inatazamiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kubadilisha tabia za usafiri wa miji mikubwa. Hebu jifikirie ukienda kazini huku unasoma gazeti bila wasiwasi. Ufikapo kazini gari linaondoka zake kwenda kwa mke wako kumpeleka sokoni, kisha linawarudisha watoto wako nyumbani kutoka shule kisha linakufuata kazini kukurudisha nyumbani. Je, imekaaje hiyo? Hakika, Google inazidi kushangaza dunia.
No Comment! Be the first one.