Suala la uhuru na usawa katika masuala ya ushindani wa kibiashara ni jambo kubwa sana katika mataifa yaliyoendelea. Kampuni ya Google kuchunguzwa huko barani Ulaya kutokana na madai ya kwamba wanapendelea apps zao tuu ndio ziwe zinakuja tayari zikiwa zimepakuliwa katika simu zinazotumia programu endeshaji ya Android.
Tume ya ushindani ya Umoja wa Ulaya (European Antitrust Commission) imefungua uchunguzi rasmi juu ya Google na mikataba yake kwa watengeneza simu zinazotumia Android mapema mwezi huu wa nne.
Pia wameishtaki Google wakidai kampuni hiyo kupitia huduma ya utafutaji (Google Search) imekuwa ikipendelea matokeo yanayohusisha huduma zake za manunuzi.
Kuna uhusiano gani kati ya apps za Google na Android?
Programu endeshaji ya Android ilikuwa inatengenezwa na kampuni ya Android, Inc – na Google alikuwa ndiye mwezeshaji namba moja kifedha kwa Android Inc.
Mwaka 2005 Google wakaamua kuinunua Android Inc na kufikia mwaka 2007 walitambulisha rasmi programu endeshaji ya Android, pia mwaka huo huo wa 2007 walitambulisha umoja ulioitwa Open Handset Alliance. Huu ulikuwa umoja wa watengenezaji software, vifaa (hardware) pamoja na makampuni ya kimawasiliano lengo kuu likiwa ni kupitia Android kutengeneza simu
Kwa nini simu za Android zinakuja na apps za Google?
Android inategengenezwa na kumilikiwa na Google huku ikijumuisha makampuni mbalimbali kama washirika katika utengenezaji wa Android ambayo wenyewe Google wamechukulia kama ni programu huru zaidi. Wakati inaingia sokoni ilikuwa na lengo la kushindana dhidi ya Apple na iOS, ambapo Apple wanasimamia vitu vingi sana kiasi cha kufanya programu endeshaji hiyo isiwe ya uhuru sana.
Kupitia Android Google walilenga kuwapa watengenezaji simu na watengenezaji softwares(apps) uhuru zaidi ukilinganisha na hali ilivyo kwa iOS.
Programu endeshaji ya Android inapatikana kwa mtengenezaji simu yeyote atakayetaka kutoa simu ikiwa inatumia OS hiyo.
Android Partners – makampuni yabanwa kwenye mikataba
Mikataba ambayo Google wanaiita siyo ya lazima, unaweza ukatengeneza simu inayotumia Android bila kuingia mkataba wa Android Partners (Washirika wa Android). Ila kuna faida mbalimbali za kuwa partner hii ikiwa ni pamoja na kushirikishwa sana katika utengenezaji na maendeleo ya programu endeshaji hiyo ya Android. Mikataba ya Android partners inasemekana inawataka kutumia apps za Google katika simu zao.
Hivyo ingawa washirika (kama vile Samsung, HTC, n.k) wana uhuru mkubwa katika maboresho ya muonekano n.k bado wanajikuta ni lazima simu zao zije zikiwa na apps za Google. Yaani ata kama Yahoo Mail yupo tayari kulipia simu ije na app yao ya barua pepe na si ile ya Gmail hilo halitawezekana.
Tatizo linakuja wapi?
Washindani wa Google wameenda kulalamika kwa chombo cha ushindani balani Ulaya ni kuhusu simu nyingi kuja tayari zikiwa na apps za Google tuu na si za washindani wake. Wakidai suala hili linaua ushindani, na kwamba Google wanaitumia Android kuzidi kujitutumua katika ukuaji wa biashara zake zingine kupitia apps zake.
Google inaweza pigwa faini ya hadi asimilia kumi ya mapato yote ya kampuni mama – ALPHABET
Kama nilivyosema awali ingawa kampuni yeyote inaweza tengeneza simu na kutumia programu endeshaji ya Android kuna vigezo kadhaa vinawabana watengenezaji wengi na kujikuta mwishoni wanaweka apps zote za Google. Mfano, uwezi chagua apps mbili tuu za Google kwa ajili ya kuweka kwenye simu, watengenezaji wanatakiwa kuweka karibia apps zote pale wanapotaka kuweka app yeyote ya Google kwenye simu hizo.
Watu waliochungulia mikataba ya Google na makampuni ya utengenezaji simu kama vile Samsung n.k wanasema Google wanabana kampuni nyingi katika eneo la apps zinazoweza kuwekwa kwenye simu hizo.
Mifano;
- Kama mtengenezaji simu alikuwa anataka kuweka App ya YouTube basi atatakiwa kuweka pia apps zingine kama vile Google Search na Google Maps ata kama kulikuwa na mshindani mwingine aliyetaka lipia app yake kuwekwa – mfano Bing Search.
- Pia kuweza ata utumiaji wa Google Play kwenye simu unawalazimisha watengenezaji hao kuhakikisha kuna apps nyingine mbalimbali za Google zinakuwa zinakuja na simu tayari zikiwa zimepakuliwa
- Kama mtegnenezaji simu anataka kuweka app ya Google Search kwenye simu basi anatakiwa pia kuweka karibia apps zingine zote, yaani Google Finance, Maps, News, YouTube, Gmail, n.k
- Pia wengi wanabanwa ya kwama ni lazima kwenye simu hizo sehemu ya ‘Home screen’ kuwe na folda la Google, ambalo mtu akilibofya liwe na apps mbalimbali kutoka Google. Hii inasemekana ni takribani apps 13, hii ikiwa ni pamoja na Google Chrome, Google Maps, Google Drivem YouTube, Gmail, na nyingine nyingi.
Hili limefanya simu nyingi kuja moja kwa moja na apps karibia zote za Google na hivyo hali kuwa ngumu kwa apps shindani kuweza kufanya vizuri ata kama nazo ni za kiwango kizuri.
Ulaya washaibana Microsoft na programu endeshaji yao ya Windows
Uchunguzi huu wa Google na Android unafanana sana na kilichowatokea Microsoft na uamuzi wao wa kuweka programu zao zaidi katika OS yao ya Windows. Mwaka 2013 Microsoft walipigwa faini ya Euro milioni 561 (Takribani Tsh Trilioni 1.3 | Ksh Bilioni 64) kwa kosa kama hili ila lilihusisha wao kuweka programu zao tuu kama vile Internet Explorer (IE). Hii ikiwa ni asilimia 10 ya mapato yao kwa mwaka wa fedha uliokwisha na Google wakikutwa na hatia watapigwa lungu hilo hilo la 10%.
Uchunguzi huu ulianzishwa mwaka 2007 pale watengenezaji wa kivinjari cha Opera walipolalamika kwa tume wakisema Microsoft wanatumia vibaya programu endeshaji yao ya Windows kwa kutowapatia wanunuzi chaguzi la kutumia kivinjari watakacho pale wanaponunua kompyuta. Microsoft wakawa wanaweka chaguzi la kivinjari utakacho pale unapowasha kompyuta kwa mara kwanza huko barani ulaya.
Google wanasemaje?
Bado Google wanajitetea wakisema hawalazimishi watengenezaji simu kuweka apps za Google na huku ata wakisema kwa data za sasa kuna simu nyingi zaidi zinazokuja bila ya apps nyingi za Google ukilinganisha na programu endeshaji ya iOS ya Apple – na Apple hawajashitakiwa.
Teknokona tutaendelea kufuatilia muendelezo wa jambo hili, ila kwa haraka haraka inaonekana itakuwa vigumu Google kuchomoka katika hili. Ingawa ni kweli kuna uhuru flani katika Android ila ukubwa wa Google unafanya kuwa rahisi makampuni mengine shindani kulalamika kuonewa kiushindani.
Je unafikiri Google anaonewa katika hili au anastahili?
Vyanzo: Imeandikwa kwa kutegemea vyanzo mbalimbali vya mtandao
2 Comments
Comments are closed.