Google (ama Alphabet) inajiandaa kutangaza kuungana na kampuni kongwe ya magari ya Marekani, Ford Motor Company kwenye maonesho ya CES mwaka huu.
Muunganiko huu ni kwa ajili ya kutengeneza magari yanayojiendesha kwa kutumia teknolojia iliyovumbuliwa na Google.
Teknolojia ya magari yanayojiendesha inazidi kukua!
Mara kwa mara kwenye mwaka ulipoita, wa 2015, teknolojia ya magari yanayojiendesha ilikuwa ikichukua vichwa vya habari. Kadri muda unavyoendelea kuenda, dhima ya magari haya mapya inageuka kuwa kitu cha uhakika na huenda magari yanayojiendesha yakaingia mitaani muda si mrefu kwenye nchi zinazoendelea.
Kampuni ya Google wanatabiria uwezekano huo kuwa kuanzia mwaka 2020, wakati kampuni nyingine maarufu kwa teknolojia hii, Tesla wakitazamia magari hayo kuanza kutumika kwa wingi kuanzia mwaka 2018.
Muungano huu unamaanisha nini hasa?
Kwa mujibu wa tovuti ya TechRepublic, muungano wa Google na Ford huenda ukaongeza ushindani katika nyanja hii ya teknolojia dhidi ya Tesla. Google tayari wamepiga hatua kubwa za kiteknolojia kwenye magari yanayojiendesha, huku Ford wakiwa na uzoefu mkubwa pamoja na imani ya wateja Marekani na kwa kiasi kikubwa Uingereza, ambayo ni soko zuri.
Chanzo cha TechRepublic kinanukuu kwamba Google inahitaji uzoefu wa Ford katika kutengeneza, kusambaza na kutangaza magari, wakati Ford wakihitaji wataalamu wa Google kupiga hatua ndefu na sababu hizi zinafanya muunganiko wao kuwa wa maana zaidi.
Muungano huu hautakuwa wa kipekee kwa Google kwani imefahamika kwa muda mrefu kwamba wamekuwa wakikutana na makampuni mbalimbali ya magari kwa ajili ya ushirikiano. Pamoja na habari hizi, imefahamika kwamba huenda Ford wakatengeneza makubaliano nje ya kampuni kuu ya Ford ili kukwepa hatari zisizojulikana za magari yanayojiendesha, jambo ambalo limekuwa na mjadala mkali kuhusu magari haya.
Makala hii ya TechRepublic inaataadharisha hata-hivyo kwamba kwa sasa muungano wa Ford na Google ni uvumi mkubwa, unaozungumziwa sana ila kuna ishara nyingi za wazi zinazoashiria muunganiko, ikiwemo mabadiliko ya watu muhimu kwenye kampuni zote mbili, nia ya wazi ya Ford kuingia katika majaribio ya biashara ya magari yanayojiendesha mwaka huu na uhusiano wa karibu wa Ford wakati Google wanatengeneza gari lao la aina ya kwanza.
Endapo kampuni hizi mbili zitaungana, ushindani kwenye utengenezaji wa magari yanayojiendesha utaongezeka, pengine kuipa wasiwasi kampuni ya Tesla ya bilionea Ellon Musk ambayo inaonekana iko mbele kwa sasa.
No Comment! Be the first one.