Miaka miwili baada ya Lenovo kununua kampuni ya simu ya Motorola kutoka Google wamesema rasmi mipango yao ya kuliondoa jina la ‘brand’ hiyo – ‘Motorola’ taratibu kuanzia hivi karibuni.
Motorola – kampuni iliyotuletea simu ya kwanza ya mkononi!
Ulikuwa unalifahamu hili? Motorola ndio kampuni ya kwanza iliyokuja na simu ya mkononi ya kwanza iliyoweza kuuzwa kwa watumiaji wa kawaida.
Baada ya miaka mingi ya mafanikio biashara ya simu ikabadilika sana miaka ya 2000, ushindani ulikuwa mkubwa na mabadiliko yalihitajika ili kujihakikishia mafanikio. Mwaka 2011 kampuni hiyo ikajivunja kutengeneza kampuni zingine mbili zinazojitegemea, Motorola Solutions na Motorola Mobility.
2012 – Motorola Mobility yanunuliwa na Google
Motorola Mobility ndio ilikuwa imejikita zaidi katika biashara ya simu, na mwaka 2012 Google walitangaza rasmi kununua kampuni ya Motorola Mobility. Wengi walioona ununuaji huu ulikuwa si kwa ajili ya biashara ya simu kwani umiliki wa Google wa programu endeshaji ya Android inayotumiwa na makampuni mengine mengi ungeingiliana na suala la wao kumiliki kampuni ya Motorola.
2014 – Google wawauzia Lenovo
Google walinunua Motorola Mobility ili kujitutumua katika umiliki wa hakimiliki za teknolojia mbalimbali ambazo zilikuwa zinamilikiwa na kampuni ya Motorola Mobility. Baada ya miaka miwili ya umiliki wa Motorola Mobility Google waliwauzia Lenovo katika dili ambalo Google walibakia na umiliki wa haki miliki wa teknolojia (Patents).
Jina la ‘Motorola’ linamiaka 86 tokea mara ya kwanza kuanza kutumika.
Moto by Lenovo: Mabadiliko gani yanakuja?
Lenovo wamesema taratibu wataacha kutumia jina zima la Motorola na badala yake wataweka msisitizo katika utumiaji wa kifupisho chake maarufu cha ‘Moto’. Na inategemewa kwenye simu hizo jina kamili la kutumika liwe Moto by Lenovo.
Lenovo wamesema simu zitakazobeba jina la Moto zitakuwa simu janja zenye sifa za juu na kwa ajili ya watumiaji wa hali ya juu huku simu za Lenovo zilizokuwa zinatumia jina la ‘Vibe’ zitaendelea kutoka ila zitakuwa za kawaida, za bei nafuu kwa ajili ya watumiaji wasiotaka simu ya bei za juu.
Ingawa Lenovo inashikilia nafasi ya juu katika biashara ya kompyuta imekuwa bado ipo nyuma kwenye eneo la simu na ununuaji wa Motorola uliwaingiza kwenye eneo hili kwa kiwango cha juu.
No Comment! Be the first one.