Mapato ya Huawei yaporomoka zaidi huku vikwazo vya kibiashara walivyowekewa na serikali ya Marekani vikionekana kuchangia zaidi tatizo hili. Ni zaidi ya miezi tisa sasa kampuni hii inakutana na kuporomoka kwa mapato katika ripoti zake.
Mapato ya Huawei yaliporoka kwa asilimia 32 katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai – Septemba 2021, wakipata Dola Bilioni 21.2 za Kimarekani. Kitengo cha bidhaa ya simu ndicho kilichoathirika sana, Huawei wakishindwa kuuza simu janja kwa wingi kama walivyowahi kufanikiwa. Watumiaji wengi wameacha kununua simu hizo kutokana na simu hizo kukosa huduma mbalimbali muhimu kwa watumiaji wa simu janja.
Huawei wanawekeza katika teknolojia na bidhaa nyingine zaidi hasa za kutumika nchini China ili kuweza kupata ukuaji mkubwa kupitia China ili kuweza kupata mapato mapya na hivyo kupunguza hasara inayotokana na kuporomoka kwa biashara yao – hasa ya simu janja na vifaa vya teknolojia ya 5G katika masoko mengine duniani. Kwa sasa wana lengo la kufanikisha utumiwaji wa programu endeshaji yao ya Harmony OS kwenye vifaa takribani milioni 200 kufikia mwisho wa mwaka.
Sekta ya biashara ya bidhaa za simu kwa watumiaji ndio iliyokuwa inakua kwa kasi kimapato na kimauzo kwa Huawei kabla ya serikali ya Marekani chini ya Rais Trump kuleta vikwazo vingi dhidi ya Huawei. Rais wa sasa pia anaonekana kutoweka kipaumbele chochote katika kuviondoa.
Huawei wamejikuta wakizuiwa kupata huduma mbalimbali muhimu kwenye simu zao ili kuweza kufanikisha mauzi ya simu hizo katika masoko mengine nje ya China. Kwa sasa ni vigumu kuuza simu ambayo watumiaji watapata shida kupata huduma muhimu kama vile soko la apps la Google Playstore, huduma ya Google Maps, na zingine zingi kutoka familia ya Google.
Vikwazo vya serikali ya Marekani viliwazuia wao kupata marighafi muhimu kutoka makampuni mengine ni mwiba mkali kwenye uwezo wa Huawei kushindana na bidhaa zingine katika soko la nje ya China. Mauzo ya asilimia 32 chini ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka mmoja uliopita ni jambo ambalo linaonesha kwa kiasi gani vikwazo hivi zimeathiri ukuaji wa Huawei.

Tayari Huawei waliuza biashara ya simu za Honor ili kuinusuru dhidi ya kuathirika na vikwazo vya Marekani.
Je unadhani bado Huawei wanaweza kutoboa kwa kuuza simu zinazokosa apps nyingi muhimu ambazo watu washazizoea? Data kwa sasa zinaonesha itakuwa ngumu, tutegemee kuona mauzo yakizidi kushuka.
Vyanzo: Time na vingine mbalimbali
No Comment! Be the first one.