Chrome na Firefox ni vivinjari wavuti vilivyokamata dunia linapoongelewa suala la kuperuzi wavuti katika miaka ya karibuni. Yapo mengi ya kutofautisha kati ya vivnjari hivi ila cha kukubaliana ni kwamba vyote viwili vinatengenezwa na maprograma wenye ujuzi wa hali ya juu kuizifanya kuwa na teknolojia ya kisasa zaidi.
Dhamira Tofauti
Jambo la kwanza kabisa katika kulinganisha Firefox na Chrome ni dhamira za msingi zilizotumika katika kuzivumbua na zinazoendelea kushikilia uhai wa vivinjari hivyo.
Chrome inatengenezwa na Google, kampuni ya kibiashara yenye dhamira ya kujua kila kitu kuhusu mteja wake ili kumpa teknolojia inayomsaidia kipekee. Kwa upande wa pili, Firefox inatengenezwa na Mozilla, asasi huru inayohusisha watu kutoka nchi mbalimbali duniani kote wanaojitolea kupambana kuitunza intaneti kuwa huru na salama kwa wote na hivyo kupingana na suala la kukusanya taarifa binafsi za watu.
Kwa kuzingatia dhamira hizo za msingi, Firefox hupendelewa zaidi na watu wanaopenda faragha na wanaohofu kuhusu kugawa taarifa zao, wakati Google Chrome hutumiwa zaidi na watu wanaotumia na mfumo wa Google na wasioona tatizo kugawa taarifa zao kwa Google.
Ulinzi na Usalama
Firefox na Chrome zinasifiwa kwa usalama.
Google hutegemea wataalamu wao wanaowalipa fedha nyingi kuhakikisha wanatengeneza kivinjari salama zaidi na wataalamu wa nje wanaosaka malipo kwa ku-hack kiungwana. Pia, wana mashindano ambapo mtu yeyote mashuhuri anaitwa kuichokoa chrome anavyojua yeye ili kuonesha ‘mapungufu’ yake ili kuzawadiwa kitita kikubwa cha fedha. Kwa upande wa pili, Mozilla ni kama jumuia ya kawaida. Ina watu mbalimbali mashuhuri ikiwemo sungusungu pia, watu ambao wana ujuzi na hamasa ya kuvumbua na kutatua masuala ya usalama. Mozilla hulindwa na sungusungu hawa kutoka kila kona ya dunia. Tatizo likigundulika, watu hulishughulikia masaa 24-wiki nzima mpaka ufumbuzi upatikane.
Muonekano na Utumikaji
Google Chrome ina muonekano mrahisi sana. Firefox ina muonekano unaolenga kumpa mtumiaji uhuru wa kuifanya ionekane anavyotaka.
Google wenyewe wanauita muonekano wa Chrome ‘minimalistic’, yani – isiyokuwa na mbwembwe. Chrome ina kijisehemu cha kuandika anuani ya tovuti, ambapo hapohapo unaweza kuandika chochote na ukaweza kukitafuta kwenye Google (kwa mpangilio wa kawaida).
Muonekano wa Firefox una kisehemu cha anuani ya tovuti na pia kipengele cha kutafuta mtandao kwa kutumia injini tofauti kama duckduckgo, Bing na nyingine nyingi zinazoweza kuongezwa. Hiki kipengele ni kwa ajili ya harakati za kuiweka intaneti huru. Kwa kuweka hiki kipengele wazi kinawaonesha watu kwamba, mbali na injini ya Google na kampuni nyingine yenye kivinjari chake, kuna injini nyingine pia ambazo mtu anaweza kutumia kutafuta chochote kwenye intaneti.
Kuanzia Firefox 30, Mozilla wameweka wazi haki ya mtu yeyote kufuta historia yake kwenye kivinjari hicho baada ya kuweka kibofya cha kufuta historia karibu zaidi na mtumiaji, kitu ambacho kinaiweka tofauti sana na Chrome, pengine na vivinjari vingine vyote.
Chrome na Firefox zote zina uwezo wa kuoanisha (‘Sync’) mipangilio yako na data kati ya vivinjari vyao kwenye simu, tableti na kompyuta na hivyo kufanya urahisi wa kuperuzi na kifaa chochote.
Huduma za Ziada na Nakshi
Ushindani mkubwa kati ya Firefox na Chrome unaweza kuwa katika kipengele hiki kama wewe ni zaidi ya mtumiaji wa kawaida.
Kuna mambo mengi unayoweza kuongeza katika kivinjari cha kisasa kwa kutumia ‘add-ons’, ‘extensions’, ‘apps’, ‘personas’ na ‘themes’ ili kukupa uwezo wa kutazama barua-pepe, sms, namba za simu, kurekebisha programu na mengineyo. Binafsi, nadhani Google wamekomaa sana katika ‘apps’ kupitia Chrome Webstore ingawa Mozilla wanajitahidi kwa kasi nzuri kuleta ushindani na Firefox Marketplace. Katika kubadili muonekano kwa ‘themes’, Firefox inavutia zaidi na katika ‘extensions’, zote mbili katika nafasi zake ziko vizuri kukupa uwezo ila kama unatumia huduma za Google kwa wingi, Chrome itakufaa zaidi.
Hitimisho
Firefox na Chrome ni vivinjari vinavyoongoza kwa ubora duniani kwa sasa. Vivinjari vyote viwili ni salama, rahisi kutumia na kuviweka vile mtu apendavyo. Mozilla na Google wanawekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha wanatumia teknolojia ya hali ya juu katika kutengeneza vitumi hivyo. Kwa kweli, hamna tofauti sana kati ya Firefox na Chrome ila tu chaguo linabaki kwa mtumiaji – Je, unapenda teknolojia ya wote, inayotamba kulinda usiri na faragha zaidi (Mozilla Firefox) au teknolojia inayokulenga wewe moja-kwa-moja kwa kutumia taarifa zako (Google Chrome).
Picha na:
www.techster.gr, www.omgchrome.com, www.cnet.com, www.elakiri.com.
No Comment! Be the first one.