Mauzo ya simu janja nchini Uchina katika robo ya nne ya mwaka 2021 yameshuka kwa asilimia 11 lakini hilo halijafanya Honor kushindwa kushika nafasi ya pili tangu itoke chini ya mwamvuli wa Huawei.
Takwimu zilizotolewa na Counterpoint (kampuni iliyojikita kufanya utafiti wa mauzo ya simu janja kwa kila robo ya mwaka) imetoa takwimu za mauzo ya simu janja kwenye soko la Uchina katika robo ya nne ya mwaka 2021. Je, nani kinara? Apple ameshikilia uskani kwa kuweza kupata 21.7% ya mauzo yote nchini humo kulinganisha na 17.1% katika kipindi sawa na hicho mwaka 2020.
Honor ambayo haipo tena chini ya mwamvuli wa Huawei kwa mara ya kwanza imeweza kushika nafasi ya pili kwa mara ya kwanza ikisimama yenyewe kwa kupata 16.7% kulinganisha na 7.5% ya mwaka 2020. Oppo imefanikiwa kuwa nafasi ya tatu kwa kupata 16.6% kulinganisha na 17.3% ya kipindi kama hicho mwaka 2020.
Vivo imekuwa ya nne kimauzo ya simu janja huko Uchina kwenye robo ya nne ya mwaka uliopita kwa kupata 16.5% ya mauzo yote ya rununu; katika kipindi sawa na hicho mwaka 2020 Vivo ilipata 17%. Nafasi ya 5 imekwenda kwa Xiaomi ambayo ilifanikiwa kuuza 16.1% (kulinganisha na 12.5% ya mwaka 2020) ya mgao mzima wa mauzo ya simu janja kwenye robo ya nne ya mwaka 2021 huko Uchina. Kampuni nyingine kwa pamoja mauzo yao yalikuwa ni sawa na 12.4% (28.6% ya mwaka 2020) ya mgao mzima.

Shukrani kwa iPhone 13 ambayo ilichagiza kupandisha mauzo ya Apple nchini Uchina. Halikadhalika, Honor Magic 3 na Magic V ziliafanya kampuni hiyo kwenda nafasi ya pili kwa mara ya kwanza ikisimama kwa kujitegemea yenyewe.

Je, mambo yatakuaje kwenye robo ya kwanza kwa mwaka huu wa 2022? Tutakufahamisha ewe msomaji wetu mara baada ya takwimu hizo kupatikana kutoka kwa mhusika.
Vyanzo: Couterpointer, GSMArena
No Comment! Be the first one.