Kwa muda mrefu watu wengi wamekuwa wakiona shirika la mawasiliano la TTCL kama shirika lililonasa katika miaka ya 1990 na ya mwanzoni wa miaka ya 2000…huku mitandao mipya ya simu ikiingia nchini na kukua kwa kasi. Hili limekuwa kiutendaji na kiteknolojia.
Ila kwa takribani miezi kadhaa sasa inaonekana shirika hilo kongwe la simu limeanza kujitutumua. Hii ilikuwa ni pamoja na kutangaza rasmi uwekezaji katika teknolojia za 4G LTE na maboresho mengine ya kiteknolojia ya mawasiliano.
Lakini pia kuna sehemu muhimu ambayo wengi wameshaiona ina tatizo muda mrefu na haikuwa haijaguswa. Nayo ni rasilimali watu – yaani wafanyakazi wa shirika hilo. Mtu yeyote ambaye ashaenda kupata huduma katika shirika la TTCL basi kwa kiasi flani anaweza kuona utofauti wa utendaji na huduma kati ya wafanyakazi wa shirika hilo na makampuni mengine ya simu.
Hivi karibuni shirika hilo lilikuja na huduma ya 4G
Ukuaji wa ushindani unaotokana na makampuni mengine ya simu moja moja inabidi kulifanya shirika la TTCL lipitie wafanyakazi wake, kuwafundisha na kuwakuza kiuujuzi na pale wanapoona wengine ni mizigo tuu kwa wakati wa sasa basi si vibaya kama litawaacha. Muhimu ni kusonga mbele.
TTCL wanauwezo mkubwa wa kiteknolojia kwa sasa na pia uwezo mwingine mkubwa zaidi wa kutumia rasilimali za kiteknolojia zilizo chini yao kwa ajili ya kuboresha huduma zao na kuzifanya ziwe za kiushindani zaidi katika soko. – ILA Kufanikiwa MAAMUZI MAGUMU yanaitajika!
Kila mtanzania nadhani angefurahi kama angetumia mtandao wa TTCL, kuna huduma nyingine kama za intaneti ambazo ni za uhakika tuu ila kwa muda mrefu inaonekana nguvu za kuzitangaza (marketing) huduma hizo na kuziboresha kiushindani hazijakuwepo sana.
Inasemekana kwa sasa shirika hilo linawafanyakazi takribani 1500 na inategemewa hivi karibuni itawabidi kupunguza wafanyakazi 400 ili kuzidi kujijengenea ufanisi. Ofisa Mtendaji Mkuu, Dk Kamugisha Kazaura alikaririwa na gazeti la Mwananchi akisema wanampango wa kupitia wafanyakazi wote walionao na kufanya tathmini. Lengo likiwa ni kuangalia jinsi gani wataalamu waliopo wanatumika kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
TTCL ni shirika lilianzishwa (1993) na kukua katika ulimwengu wa huduma za simu za mezani – mabadiliko ya teknolojia na ukuaji wa huduma za simu za mkononi na intaneti hayakupokelewa na kutangazwa kwa kasi iliyoitajika.
Kama mabadiliko hayo yangepokelewa vizuri na huduma kutolewa na kutangazwa kwa kasi basi TTCL ingekuwa moja ya makampuni 3 ya juu nchini Tanzania. Au unaonaje?
Vyanzo: Mwananchi na vinginevyo