Wana teknolojia siku zote huwa wanabudi vitu vya aina yake na wanatumia mbinu kadha wa kadha katika kuhakikisha vitu hivyo vinatumika au vinawaunganisha hata wale ambao hawapendi teknolojia kwa kiasi kikubwa.
Kitambo hicho makampuni mengi yalikuwa yakicheza na majina ya ‘Software’ zake katika kutofautisha matoleo. Kwa mfano kampuni kama Apple na Microsoft zilikuja na majina tofauti tofauti ya kuzipa ‘Software’ hizo (Os). Microsoft ilikuja na Windows 95, Windows 98 ambayo mtiririko huu kwa namna moja au nyingine unaboa hivi. Baada ya muda kidogo wakaja na majina mengine kama vile Windows Xp, Windows Vista lakini wakarudia asili yao ya kutoa majina na kwenda kwenye Windows 10.
Ukiangalia kwa upande mwingine kampuni la Apple lilikuwa na ubunifuu zaidi juu ya jambo hili. Os zake zilikuwa na majina ya kipekee kama vile ‘Cheetah’ , ’Lion’, ‘Snow Leopad’, ‘Jaquar, na ‘Puma’.
Kampuni lingine ambalo linajipa umakini mkubwa katika kuzipa Os zake majina ni Google. Jinsi wanavyopangilia na kutoa majina kwa Os za Android kwa ajili ya simu limekuwa ni swala la aina yake na linaloongelewa sana na watu.
Google imezipa majina Os za Android kutoka kwenye majina ya peremende. Kwa Ufupi ilianza na:
- CupCake (Android 1.5)
- Donut (Android 1.6)
- Eclair (Android 2.0/2.1)
- Froyo (Android 2.2/2.2.3)
- Gingerbread
- Honeycomb (Android 3.0)
- Ice cream
- Jelly Bean (Android 4.1)
- KitKat (Android 4.4)
- Lollipop (Android 5)
- Marshmallow (Android 6)
Kwa haraka haraka kama unavyoona ni kwamba majina ya peremende hizi yameanzia katika herufi C na kuendelea (kwa sasa imefikia katika herufi M). Watu wengi wanajiuliza kwa nini hawakuanza na herufi A ikafuatiwa na B, lakini wakaruka mpaka C. Majibu tofauti tofauti yamekuwepo na kati ya hayo ni kwamba labda matoleo ya mara ya kwanza yalikuwa ni yale ya ‘Alpha’ na ‘Beta’ (inavyosemekana)
Swali lingine ambalo wamekuwa wakiulizwa sana ni kwamba kwa nini wameamua kutoa majina hayo kutoka katika peremende tofauti tofauti lakini hakuna hata mfanyakazi mmoja alieweza kutoa majibu. Hata msemaji wa Google alipoulizwa alijibu kwa kusema kuwa hilo ni jambo la ndani ya kampuni zaidi.
Swali toka TeknoKona je, watakapofika mpaka kwenye herufi Z matoleo yatakayofuata yatakuwa yanaanzaje? Maana ukifuatilia mtiririko vizuri ni kwamba kampuni linachagua majina ya peremende lakini peremende hizo zinapangiliwa katika mtiririko wa A – Z (kwa sasa Os ipo kwenye herufi M). Labda tungoje wote tuone……