Mitandao ya simu ina utaratibu wa kuleta simu spesheli kwa wateja wao zinazokuwa zinauzika kwa bei nafuu ukilinganisha na zile zinazouzwa na makampuni ya utengenezaji simu. Mtandao wa Vodacom umekuja na simu janja inayoitwa Vodocom Smart 6.
Vodacom Smart 6 inapatikana kwenye maduka ya Vodacom kwa bei ya Tsh 90,000/=, na ukinunua simu hii unapata MB 500 na SMS 200 kila mwezi kwa muda wa miezi sita. Kwa kiasi kikubwa ili ni dili linalovutia.
Unaweza pia kuangalia uchambuzi mzima kupitia video tuliyoiweka kwenye akaunti yetu ya YouTube –
Sifa za Vodacom Smart 6
Diski ujazo wa GB 4 – Simu hii inakuja na diski ujazo wa GB 4, ujazo huu ni mdogo kwa mtu mwenye matumizi mengi na ni kwa sababu hii ndio maana inakuja na eneo la kutumia memori kadi (SD Card).
Android 4.4.2 – Vodacom Smart 6 inatumia programu endeshaji ya Android 4.4.2, Kit Kat. Ili ni toleo la kisasa la Android na linakuwezesha kufurahia apps karibia zote zinazopatikana katika soko la apps la Google
Kamera – Inakuja na kamera moja tuu, ya nyuma. Kamera hii ina megapixel 2 na hakuna flash. Kwa matumizi ya kawaida ya picha moja moja kwa ajili ya kutuma WhatsApp na kwingineko basi itatosha ila haitakufaa kama unaitaji picha za kiwango kikubwa cha ubora.
Betri – mAh 1400, kwa kuwa ni simu nyepesi na kwa mategemeo ya kutumiwa kwa matumizi madogo – yaani kwa ajili ya mawasiliano zaidi na hii ikiwa ni pamoja na matumizi ya apps kama vile Facebook, WhatsApp, Instagram na Twitter, kiwango chake cha uwezo wa chaji wa betri unajitosheleza. Nimetumia kwa zaidi ya siku nne na ninaweza kusema ukiichaji hadi kujaa basi kwa matumizi ya kawaida basi tegemea zaidi ya masaa 24 ya utumiaji baada ya kuchaji.
Apps – Vodacom Smart 6 inakuja ikiwa tayari na apps mbalimbali muhimu hii ikiwa ni pamoja na Facebook, Gmail, Soko la apps la Google Play, na Twitter. WhatsApp ndio app inayokosekana ila utaiweza ipata mara moja kwa urahisi kupitia soko la apps la Google Play.
Tunasemaje?
Kama unataka kununua simu janja yenye umbo dogo na isiyo ya gharama na tayari ni mteja au unataka kujiunga na Vodacom basi simu hii ni chaguo sahihi. Pia Vodacom Smart 6 inaweza ikawa ni simu nzuri kuwa kama zawadi kwa mtu ambaye hajawahi kutumia simu janja kabla au kwa mtu ambaye anaitaji simu kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kila siku – yaani kupiga na kupokea simu, apps kama WhatsApp, Twitter n.k.
One Comment