Watanzania na waafrika wana sababu nyingine ya kufurahia teknolojia. Baada ya simu kadhaa kuingia kwenye soko la Afrika kutoka Nokia, Android na China, shirika la intaneti la Mozilla nalo limetangaza kuleta simu-janja zenye bei nafuu zaidi ya ilivyowahi kutokea.
Shirika la Mozilla linajulikana zaidi kwa kivinjari-wavuti cha Firefox, hatahivyo limejikita kuhakikisha intaneti inabaki huru na salama kwa dunia nzima. Katika kuendelea kutekeleza azima hiyo, Mozilla wanaleta simu zinazobeba mfumo-endeshaji wa Firefox OS ambayo inatokana na kivinjari wavuti chao.
Tayari Mozilla imefanya majaribio ya simu zake nchini India na bara la Asia, ambako pia wameshirikiana na watengeneza simu wa ndani wa nchi hiyo kutengeneza simu zenye bei ya kutupwa ya kuanzia dola 25 za kimarekani (TShs. 42, 600).
Hapa Afrika, Mozilla wamepata ushirikiano kutoka kwa Airtel na Tigo, ambazo pia zinapatikana hapa Tanzania na Afrika ya mashariki, pamoja na MTN ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini kuwa kampuni za kwanza kuleta simu zao barani Afrika.
Aina za simu zinazotegemewa
Simu zilizouzwa tayari na Mozilla ni simu za Alcatel Onetouch Fire, ZTE Open II na Intex na Spice, amabazo ni kampuni za India.
Unachoweza kufanya na simu za Firefox OS
Imeripotiwa na PC Advisor kwamba simu hizi zimetengenezwa kwa sababu za msingi za kutumia intaneti ikiwemo programu za Facebook, Twitter na Wikipedia pamoja na uwezo wa kawaida wa simu za kisasa kama kuperuzi wavuti, kutuma barua-pepe, kucheza muziki wakati unafanya vitu vingine na kuchukua picha.
Lini zitakuja hizi simu
Hivi karibuni. Kwenye blogu ya Shirika la Mozilla, hawajaweka wazi lini na wapi simu za Firefox OS zitaonekana kwa mara ya kwanza Afrika zaidi ya kusema kwamba zitakuja hivi karibuni.
Ujio wa simu za Firefox OS ni habari nzuri kwa Afrika kwa sababu mbalimbali, ikiwemo tegemeo kuenea zaidi kwa teknolojia nafuu ya mawasiliano ya kiganjani ukizingatia uchumi wa nchi nyingi, uhuru zaidi kutoka nchi za ughaibuni (Mozilla ni shirika, la kidunia zaidi na si kampuni ya nchi fulani) na kufunguka kwa fursa nyingi zaidi za kimaendeleo kwa vijana kwa kukuza mfumo uendeshaji wa Firefox OS ya simu hizo.
No Comment! Be the first one.