Tangia kampuni la Apple litangaze toleo la iPhone SE watu wamekuwa wakijikuta katika tatizo la uchaguaji juu ya simu gani kati ya iPhone SE na iPhone 6S wanunue.
Ili kukabiliana na tatizo hili la kuumiza kichwa juu ya simu gani ya kununua kati ya hizi mbili basi nimekuandalia maswali kadhaa ya kujiuliza ambayo yatakusaidia kuchagua simu yako ya kununua.
1. Kama Hutaki Kutumia Gharama Kubwa Katika Kununua Simu
Taarifa iliyopo ni kwamba iPhone 6s inauzika kwa takribani dola 750 za kimarekani. Kwa haraka haraka hii ni namba kubwa sana kwa mtu wa hali ya chini au hata Yule mwenye kipato cha kati. Sawa mwingine anaweza akajibana bana mpaka akafikia kiwango hichi cha pesa.
Lakini kuna wengine kutumia pesa nyingi ili kumiliki simu kali waonaona kama sio kitu kizuri kwao . Wanaona kufanya kazi kwa bidii ili kuchekelea mwisho wa mwezi ni kitu kizuri lakini sio kwakukusanya pesa hiyo na kuiweka katika simu (nadhani unanielewa).
iPhone 6s inauzwa dola za kimarekani 749 (ambazo ni sawa na 750 kwa akili ya kawaida) na hiyo ni kwa zile zenye GB 64. Na kama utataka zile simu kubwa kabisa kutoka katika kampuni hilo kama vile iPhone 6s plus gharama inaweza panda kwa kiasi kikubwa tuu.
Ukija kuangalia katika simu za iPhone SE, simu hizi zinaanzia kuuzwa kwa kiasi cha dola za kimarekani 399 na hii ni kwa zile zenye ujazo wa uhifadhi wa GB 16. Simu hizi ni nzuri na zina kila kitu, kitu cha muhimu cha kuweka akilini ni kwamba usikubali kununua simu yoyote kutoka kampuni la Apple ambayo ina ujazo wa GB 16 — ujazo huo kamwe hauwezi ukatosha — labda kama wewe utakuwa hupendi kuweka vitu katika simu yako hiyo.
iPhone SE ya GB 64 inauzwa kwa dola 499 za kimarekani, hili naomba liwe chaguo lako sahihi kama mfuko unaruhusu. Usiangalie udogo wa simu hizi. Sawa simu hizi ni ndogo lakini ufanisi wake ni sawa sawa tuu za zile iPhone 6
2. Unataka Kifaa Kipya Kilichoingia Sokoni
Kama unataka kumiliki simu mpya ambayo ndio imeingia sokoni bado iPhone SE ni chaguo lako. Simu hii ina mambo mengi na kama nilivyosema katika swala zima la ufanisi simu hii ina ufanisi sawa sawa na iPhone 6.
3. Kama Unataka Simu Inayodumu Na Chaji Kwa Muda Mrefu
Kiwango cha ukaaji na chaji kati ya iPhone 6S na iPhone SE vyote ni sawa ila tunaamini kwa udogo wa kioo chake (display) kuna uwezokano mkubwa wa kiwango cha chaji kwa iPhone 6S kuwahi kushuka zaidi ukilinganisha na cha kwenye iPhone SE pale utumiaji wa namna moja ukifanyika. Hila hapa kwa kiasi kikubwa ni ngoma droo…
4. Kama Unahitaji Simu Yenye Umbo Dogo
Haijalishi kama una mikono midogo, mikubwa au hata ile ya kati. Muda mwingine unaweza ukajikuta tuu kuwa unataka simu yenye umbo dogo. Umbo dogo ni zuri kwani litakuwezesha kufikia kila pande ya simu yako kwa mkono wako. Kuna simu zingine ni kubwa kiasi kwamba huwezi kuitumia vizuri mpaka ushike kwa mikono miwili.
Sawa kuna mambo kadhaa unaweza usiyapate ukiwa na iPhone SE ambayo yapo katika iPhine 6s kama vile uwezo wa ‘3D Touch’, kamera ya mbele imeshusha uwezo wake mpaka MP 1.2 na pia simu hizo hazipatikani kwa ujazo wa GB 128 kwani GB zake zinaishia katika GB 64.
Kwa haraka haraka iPhone SE ni chaguo zuri kwa mwanachi wa hali ya chini na ya kati. Kumbuka unapata mambo mengi yaliyo katika iPhone 6 ndani ya simu ndogo kabisa (iphone SE).
Niambie na wewe kama mwana Teknolojia nini ushauri wako juu ya jambo hili, je wewe unaona ni sawa kabisa? Niandikie sehemu ya comment hapo chini. Tembelea mtandao wako pendwa wa TeknoKona kila siku kwa habari moto moto za teknolojia kwa ujumla. Kumbuka TeknoKona Daima Tupo Nawe Katika Teknolojia!.
Sahihisho: Sehemu nyingi iPhone SE iliandikwa kama iPhone 5SE – ‘iPhone 5SE’ ni codename iliyokuwa inatumika kabla ya simu hiyo kutambulishwa rasmi kama iPhone SE.