fbpx
TeknoKona Teknolojia Tanzania
Facebook Intaneti Teknolojia

Je, Free Basics Ni sawa?

Je, Free Basics Ni sawa?

Spread the love

Kuna mdahalo muhimu sana unaendelea huko mtandaoni ambao pengine watu wengi hawaujui na unahusu upatikanaji wa intaneti bure kwa watu wasioweza kununua intaneti. Mpango huu tata unaitwa Free Basics (zamani internet.org). Free Basics unalenga kuwapa mabillioni ya watu katika nchi zinazoendelea uwezo wa kupata huduma za msingi za intaneti kama taarifa za habari, taarifa za kazi, taarifa za wakinamama wajawazito na elimu bure mtandaoni. Tuangazie Free Basics imetoka wapi na sababu zinazofanya mpango huu kukataliwa na baadhi ya watu na makampuni.

Free Basics Imetoka Wapi?Internet.org-app-1

Mpango wa Free Basics ulianza kama internet.org, ukiasisiwa na billionea wa Facebook, Mark Zuckerberg, ambaye pamoja na kampuni yake, wanaendelea kuisukuma kwenye nchi za dunia ya tatu. Free Basics tayari inapatikana kwenye nchi kadhaa Afika , bara la Amerika ya kusini na Asia ambapo kuna watu masikini zaidi duniani. Hapa kwetu Afrika ya Mashariki, Free Basics inapatikana kupitia mitandao ya simu wa Tigo Tanzania na Airtel nchini Kenya. Zaidi ya kupata taarifa muhimu, watu wanaweza kuwasiliana kwa kutumia Facebook na Messenger ya Facebook bure bila kuwa hata na shilingi moja kwenye simu zenye uwezo wa intaneti na zile zisizokuwa na intaneti kwa njia ya Facebook kwa SMS. Ni muhimu pia kutaja kwamba Free Basics inaungwa mkono na makampuni mbalimbali makubwa kama Intel na Samsung. Hata-hivyo, kuna wimbi kubwa la makampuni na watu mbalimbali kwenye nchi mbalimbali duniani wenye hofu kubwa kwamba Facebook itawaweka watu wanaolenga kuwaleta kwenye intaneti kwa mara ya kwanza katika sehemu mbaya na kwamba Free Basics itaminya uhuru na usawa kwenye mtandao wa intaneti.

Free Basics Inaminya Uhuru na Usawa wa Intaneti

Sehemu muhimu ya mdahalo wa kuhusu Free Basics ni suala la uhuru na usawa wa intaneti ambalo tafsiri yake ni kwamba: Mtu yeyote aliyeamua kutoa huduma ya intaneti anapaswa kuitoa bila kupendelea huduma fulani. Huduma zote zinatakiwa kuchukuliwa sawa. Inaripotiwa kwamba mnamo mwezi Octoba 2015, kampuni 65 kutoka nchi 31 tofauti duniani zilisaini barua ya wazi kwa facebook kupinga mpango wao wa Free Basics kwa kusema kwamba, “Mpango huo unaenda kinyume na misingi ya usawa wa intaneti, uhuru wa kujieleza, usawa wa fursa, usalama, faragha na ubunifu.”

SOMA PIA  Bei za Galaxy S21, S21 Plus na S21 Ultra kwenye maduka ya Tigo

Huko India napo, ambapo Facebook wanapambana na wanaharakati, huduma mbalimbali muhimu zimejitoa kwenye mpango wa Free Basics kwa madai kwamba na wao pia wana-amini kwamba mpango huo unaminya uhuru na usawa kwenye mtandao wa intaneti.

Wanaharakati hao wengi wametengeneza hoja kwamba Mark Zuckerberg na Facebook wanashindwa kuelewa kiundani hali ya kiuchumi ya watu masikini ambao Facebook inatamani kuwaingiza mtandaoni kwa mara ya kwanza. Wanasema kwamba, wengi wao wanaweza wasilipie kabisa huduma zaidi na kuona inteneti zaidi ya ile wanayopewa bure, ya Free Basics na hivyo kubakia kudhani kwamba mwisho wa intaneti ni kile wanachikiona na kukizoea kwenye Free Basics. Wanaharakati wanadiriki kusema kwamba Facebook inajijengea ukuta wake wa kipekee kwenye intaneti na kile wanachosimamia siyo intaneti ya bure, bali facebook-neti ya bure na kwamba kitu hicho hakitakiwi.

Free Basics Si salama na Inahatarisha Faragha.

Sehemu nyingine ya mdahalo wa Free Basics ni kwamba Facebook inaripotiwa kutotumia HTTPS na TLS, ambazo ni taratibu zinaotumika sana kwenye usalama wa mtandaoni. Pia, zaidi ya hapo kuna wale wenye wasiwasi na usiri wa Facebook juu ya sera ya Free Basics. Wanahoji kuelewa jinsi gani Facebook watapambana na serikali pamoja na makampuni mbalimbali yanayoipa ‘tafu’ Free Basics, katika kulinda ufaragha wa taarifa za watumiaji. Facebook bado hawajatoa taarifa muhimu juu ya hoja hii.

SOMA PIA  Sailfish OS yawa Programu endeshaji rasmi ya simu nchini Urusi

Free Basics ni Sawa – Mark Zuckerberg wa Facebook.internet-org_

Wakati wanaharakati mbalimbali wakizidi kuikaba koo Facebook juu ya Free Basics, Mtendaji mkuu wa Facebook Mark Zuckerberg ameendelea kuutetea mpango huo kwa kusema kwamba anafurahi kuona kwamba wapinzani wa mpango huu nao wana dira ya kusaidia kuwaweka watu billioni waliosalia duniani ambao hawajajiunga kwenye mtandao – kwa lengo la kuwasaidia kujikwamua kimaisha.

Mark anaamini kwamba kuwapa watu huduma za msingi kwenye intaneti bure kutasaidia kupambana na umasikini. Pia anaamini kwamba kulinda uhuru na usawa wa kwenye intaneti ni jambo muhimu linalotakiwa kuwekewa mkazo.

Mark ametoa mfano kuelezea dhana yake kwamba, “ukitaka kuuza ma-apple na ukamuuzia mzungu kwa dola moja lakini kwa mtu mweusi ukamuuzia kwa dola 2, hilo ni kosa na linafaa kukemewa na kuzuiwa.” “Uminyaji wa usawa wa intaneti uko kama hivyo. Ila kama kuna mtu anayeuza ma-apple na anataka kutoa ma-apple kadhaa kwa ajili ya msaada, hapo hakuna sheria ya kuzuia hilo. ni ngumu kuona jinsi internet.org (Free Basics) inamuumiza mtu yeyote.”

Zuckerberg anasema kwamba kwa kila watu kumi wanaotumia intaneti kwa mara ya kwanza, mmoja anainuliwa kutoka kwenye ufukara.

Facebook wafanya Maboresho kwenye Free Basics

Kujibu wasiwasi wa wadau mbalimbali, facebook imefanya marekebisho na inaendelea kufanya hivyo. Wameongeza usalama na wamefungua milango ya Free Basics kwa kutoa nyenzo za kuprogramu (API) kwa ajili ya huduma zozote zinazotaka kujiunga na Free Basics kufanya hivyo ila bado huduma hizo lazima zipitishwe na Facebook.

 

Mibadala Ipo

Watu wanaoipinga Free Basics ya Facebook wanaamini kwamba upo uwezekano wa kuwapa watu bilioni 3 ambao bado hawaijui intaneti uwezo wa kujikwamua kwa kupata intaneti bure au wanayoweza kuilipia kwa gharama iliyo karibu sana na bure.

Mfano wa mipango kama hii ya mbadala ni huduma kutoka kampuni iitwayo ‘Jana’. Kupitia app yao ya androidi ya mCent, Jana wanawapa watu fedha ya kununua intaneti kama watawatapakua app zinazotangazwa na Jana au kushirikisha mtu mwingine kutumia app hizo. ‘Jana’ wamekuwa wakishirikiana na makampuni mbalimbali ya simu na mawasiliano tangu mwaka 2006 kuupanua mpango huu duniani kote na kwa Afrika ya Mashariki, tayari wamefika Kenya.

SOMA PIA  Jacquard: Jaketi janja kutoka Google na Levi's

Wapo watu wengine wanaoshughulikia mfumo mwingine tofauti kabisa wanaotegemea utakuwa wa intaneti mpya kwa kutumia ‘Mesh Networking’. Mesh Networking inaondoa dhana ya kuwa na kampuni au watu wenye mamlaka ya kutoa huduma ya intaneti kwa watu wengine. Intaneti inayotakana na Mesh Networking inasemekana kuwa ya haraka, inayo-aminika na ya gharama nafuu zaidi.

 

Mozilla Waja Na Lao

Mwenyekiti wa asasi ya Mozilla, Bi Mitchell Baker

Mwenyekiti wa asasi ya Mozilla, Bi Mitchell Baker

Asasi inayoshughulika na u-harakati wa kuiweka intaneti huru, The Mozilla Foundation nayo ina mbadala wake wa kuwaleta watu masikini zaidi duniani kutumia intaneti kujikwamua. Mpango wao wameuita ‘Equal Rating’ – ambao unawapa watu intaneti ya bure iwapo watanunua simu ya bei ya chini kabisa ya Orange Kliff inayoendeshwa na programu-endeshaji ya Firefox OS. Simu hiyo inayouzwa kwa bei ya chini ya dola 40 za kimarekani (karibu Tsh 80, 000). Pia katika mpango mwingine wanaoufanyia majaribu nchini Bangladesh kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Grameephone, Mozilla wanawapa watu intaneti ya bure kwa kujitolea kuangalia matangazo mtandaoni.

Mwenyekiti wa asasi ya Mozilla, Bi Mitchell Baker anaendelea kufanya mazungumzo na Waziri mkuu wa India, akiweka wazi msimamo wa Mozilla juu ya mipango ya Facebook ambayo wanaona inaminya uhuru na usawa mtandaoni.

Je, wewe unafikiriaje mdahalo huu unaoendelea? Je, facebook wako sawa kutoa intaneti ya bure kwa baadhi ya huduma za intaneti wanazochagua au kuwepo na mbadala?

 

Picha Na MEDIANAMA

ecay

Ninafuatilia teknolojia kila siku na ninapenda kutoa ujuzi wangu kuhusu teknolojia. Karibu tuzungumze kuhusu teknolojia hapa teknokona!

Comment

Comments

  1. […] post Je, Free Basics Ni sawa? appeared first on […]

Leave a Reply

Your email address will not be published.

TeknoKona Teknolojia Tanzania